Na Mwandishi Wetu, dev.kisakuzi.com-Dodoma
MAMIA ya watu wakiwemo viongozi, Wanachama wa CCM na wananchi wa Dodoma wameshiriki katika mazishi ya aliyeliyekuwa Ofisa Mwandamizi wa Chama, Gordon Mwakitabu yalioongozwa na Katibu Mkuu wa CCM, Wilson Mukama.
Pamoja na Mukama mazishi hayo yamehudhuriwa na Makatibu Wakuu wastaafu wa CCM, Philip Mangula, Yussuf Makamba, Naibu Katibu Mkuu wa CCM (Bara), John Chiligati, na Makatibu wa Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Nape Nnauye (Itikadi na Uenezi), Asha Abdallah Juma (Oganaizesheni), Mwigulu Nchemba (Uchumi na Fedha) na Januari Makamba (Mambo ya Nje) na viongozi mbalimbali wa CCM kutoka Dodoma na baadhi ya mikoa.
Mazishi ya Mwakitabu aliyefariki Jumamosi mjini hapa, yalianza kwa mwili wake kuagwa na aombolezaji nyumbani kwake, Area C mjini hapa na kufuatia maziko kwenye makaburi ya Nkhungu nje kidogo ya mji wa Dodoma.
Akitoa salamu za rambi rambi, Katibu Mkuu Mstaafu Mangula alisema, Mwakitabu ni miongoni mwa wasomi wa kwanza wa elimu ya Chuo Kikuu walioajiriwa na CCM katika mkakati wa kukiimarisha Chama miaka yq 1986.
“Kwa muda wa miaka kumi niliyofanya naye kazi akiwa Katibu Myeka wangu, nashuhudia hakua mtu wa maneno bali wa vitendo, ukitaka afanye kazi wewe unampa karatasi yenye maelekezo mafupi, lakini kazi atakayokurudishia utadhani alikuwa katika akili yako wakati unawaza kazi uliyomtuma”, alisema Mangula.
Naye Katibu Mkuu Mstaafu, Makamba alisema, Mwakitabu alikuwa mchapakazi mvumilivu hata mkuu wake wa kazi angekuwa na kero kiasi gani.
“Wengi mnanijua kama mara nyingi huwa mkali na mkorofi kazini, lakini mara nyingi Mwakitabu alinifanya nijiombe radhi kumuudhi mtu mpole kama yeye, maana nilikuwa hata nikimfokea vipi yeye anaendelea kunitazama na kutekeleza maagizo kwa upole na tabasamu”, alisema Makamba.
Kwa upende wake katibu Mkuu wa CCM, Mukama alisema, alimfahamu Mwakitabu kuwa ni mchapakazi tangu mwaka 1986 wakati alipomsaili kwa ajili ya kupatiwa ajira kwa mara ya kwanza CCM baada ya kuhitimu Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Alisema, na hata baada ya kuwa naye kama Katibu Myeka wake aliendelea kushuhudia uchapakazi wa Mwakitabu kiasi kwamba anamhesabu kuwa alikuwa hazina mahsusi ya Chama kutoka kwa Mwenyezi Mungu.
Mukama alisema, kutokana na msiba huo Chama kimeguswa mno na Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete amemtuma salam nyingi za rambi rambi kwa ndugu, Jamaa, Marafiki na waliokiwa wafanyakazi wenzake Mwakitabu.
Alisema pamoja na CCM kugharamia mazishi yote kwa jumla lakini Mwenyekiti wa CCM, Rais Kikwete na CCM kwa jumla watatoa rambi rambi ambayo watamkabidhi mke wa marehemu.
Akimzungumzia Mwakitabu, Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape alisema baadaye kwamba, kujitokeza kwa viongozi na watu wengi kwenye mazishi yake, na wengi wakionyesha kugubikwa na majozi, ni dalili tosha kwamba sifa alizopewa Mwakitabu kuwa alikuwa mchapakazi ni za kweli.
“Tunajua baadhi ya sifa ambazo hutolewa kwenye misiba nyingine huwa za kupamba, lakini hizi alizopewa Mwakitabu ha viongozi hawa zinaonekana kuwa ni za kweli kwa sababu hata mimi namfahamu, kweli Mwakitabu alikuwa mchapakazi tena asiyeendekeza majungu kazini”.
Miongoni mwa viongozi waliopata fursa ya kutoa salam ni viongozi wa CCM kutoka mikoa mbalimbali ambapo pamoja na salam walitoa mchango wa ubani kwa niaba ya mikoa yao.
Kadhalika wabunge wa CCM akiwemo mmoja wa CHADEMA, Ernest Siinda waliwakilishwa na Mbunge wa Mchinga, Saidi Mtanda ambaye baada ya kutoa salamu za rambirambi alikabidhi ubani wa zaidi ya sh. milioni moja kwa familia ya marehemu.
Marehemu Mwakitabu ambaye amefanya kazi ya Katibu Myeka katika Ofisi ya Katibu Mkuu wa CCM, kwa zaidi ya miaka 15 hadi anafariki, ameacha mjane na watoto watano.