MAKAMU wa Rais wa Kenya William Ruto anakwenda The Hague, Uholanzi, ikiwa ni siku moja kabla ya kuanza kesi inayomkabili katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu dhidi ya Binaadamu (ICC) mjini humo. Ruto mwenye umri wa miaka 46 anakabiliwa na mashitaka ya kuandaa machafuko ya baada ya uchaguzi mkuu wa 2007 ambapo mamia ya watu waliuwawa. Kiongozi huyo ni mwanasiasa wa ngazi ya juu kabisa aliye madarakani kuwahi kufika mbele ya mahakama hiyo ahadi sasa na kesi hiyo itaanza siku chache tu baada ya wabunge nchini Kenya kupiga kura kujitoa katika mahakama na kuwa nchi ya kwanza kuchukua hatua hiyo.
Wakati akiondojka kwenye uwanja wa ndege wa Nairobi, Makamu huyo wa rais aliupungia mkono umati uliokuweko uwanjani, lakini alikataa kusema chochote. Ruto anatuhumiwa kupanga baadhi ya machafuko yaliozuka baada ya uchaguzi 2007-2008 ambapo watu wapatao 1,100 waliuwawa na zaidi ya 600,000 kupoteza makaazi yao.
Mshitakiwa mwenzake, mtangazaji wa kituo kimoja cha Redio Joshua arap Sang anayetuhumiwa kuratibu mashambulizi hayo, tayari yuko The Hague, ambako aliwasili mwishoni mwa juma. Wopte wamesema watakana mashtaka yanayowakabili. Jumapili Ruto alishiriki katika sala ya maombi kanisani akiwa pamoja na Rais Uhuru Kenyatta ambaye pia anatuhumiwa kuandaa kampeni ya mauaji, ubakaji na kuwahamisha watu. Kesi dhidi yake itaanza Novemba 12. Hata hivyo Rais Kenyatta amesema hatokubali yeye na naibu wake wawe nje ya Kenya kwa wakati mmoja.
“Tutashirikiana na mahakama ya ICC na wakati wote tumekuwa tukiahidi kufanya hivyo,” aliuambia mkutano wa hadhara wa wafuasi wake kwamba lazima ifahamike lakini kwamba Kenya ina katiba na kwamba Ruto na yeye hawatokuwa nje ya nchi wakati mmoja.
Kenyatta ambaye pia atayakana mashtaka yanayomkabili amesema ni ya uwongo na yatafutwa, akiongeza kwamba wapangaji wa njama hizo watatajwa na kuaibishwa. Huku akishangiriwa na umati uliokuwa ukimsikiliza, Kenyatta alisema,”shindi hautokuwa wa Ruto, Sanga au wangu , bali kwa Kenya.”
Uchaguzi wa 2007 nchini Kenya uliangamwa na madai ya wizi wa kura na mizengwe, lakini kile kilichoanza ghasia za kisiasa kikageuka kuwa wimbi la mauaji ya kikabila na mashambulizi ya kulipiziana kisasi, yakiwa machafuko mabaya kabisa tangu huru wa nchi hiyo 1963.
-DW