Wilaya ya Rombo Kudhibiti Gongo Ndani ya Miezi Mitatu

Moja wapo ya mitambo ya Gongo.

Moja wapo ya mitambo ya Gongo.


Na Yohane Gervas, Rombo

SERIKALI wilayani Rombo imesema itahakikisha inadhibiti utengenezaji wa pombe haramu ya gongo ndani ya miezi mitatu kuanzia sasa pamoja na pombe zingine za kienyeji na kulifanya tatizo la utengenezaji wa gongo kuwa historia katika wilaya hiyo.

Hayo yameelezwa na Mkuu wa Wilaya ya Rombo, Lembrice Kipuyo wakati wa operesheni ya kudhibiti utengenezaji wa pombe haramu ya gongo iliyoendeshwa katika Tarafa ya Tarakea ambapo imekua na mafanikio makubwa baada ya kukamata kiasi cha lita mia nne za Gongo.

Operesheni hiyo pia imesababishwa kukamatwa kwa mitambo 40 ya kutengeneza pombe pamoja na mapipa 1,200 ya Gongo katika Kijiji kimoja peke yake cha Kikelelwa kwa kipindi cha miezi miwili.

Kipuyo alisema kuwa endapo wananchi watashirikaina kikamilifu na kamati za ulinzi na usalama ngazi ya kijiji na kata kwa pamoja wataweza kudhibiti tatizo hilo ambalo kwa sasa limekua ni changamoto kubwa wilayani hapa.

Alisema kuwa lengo la operesheni hiyo ni kudhibiti utengenezaji na uuzaji wa pombe ya gongo kwani imekua na madhara makubwa kwa watumiaji wake kutokana na kutokana na utengenezaji huo wa pombe haramu kutofuata kanuni za afya ya binadamu na hivyo kuathiri watuamiaji wake ambao wengi wao ni vijana.

Pia katika kutoa hamasa mkuu huyo wa wilaya alitoa zawadi ya kiasi cha shilingi laki moja kwa viongozi wa kijiji hicho cha kikellelwa kwa jitihada na ushirikiana wao waliouonyesha wakati wa operesheni hiyo.

Operesheni ya kudhibiti pombe haramu ya gongo wilayani Rombo inaendelea katika vijiji vyote vya wilaya ya Rombo ili kuhakikisha hali hiyo inamalizika