WILAYA YA GEITA KUTENGA MILIONI 50 KWA MAFUNZO KUBORESHA KILIMO

Mkuu wa Wilaya ya Geita Herman Kapufi akizungumza wakati akifungua  mafunzo ya siku moja kwa maofisa ugani  wa wilayani yake wilayani humo jana yaliyoandaliwa na Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH),  yenye lengo  la kuwakumbusha wataalamu hao wa kilimo nafasi yao pamoja na kuwapatia mbinu mpya za kisasa katika kulima mazao ya Mihogo, Pamba na Viazi vitamu katika kuelekea serikali ya viwanda.

Picha ya pamoja.
Maofisa ugani wakiwa kwenye mafunzo hayo.
Mratibu wa Jukwaa la bioteknolojia kwa maendeleo ya kilimo nchini OFAB bwana Philbert Nyinondiakizungumza kwenye ufunguzi wa mafunzo hayo.
Mshauri wa Jukwaa la Masuala ya Bioteknojia OFAB, Dk.Nicholaus Nyange (kushoto), akitoa mada kuhusu matumizi ya Bioteknolojia katika kilimo.

Na Dotto Mwaibale, Geita

HALMASHAURI ya Wilaya ya Geita Mkoani Geita imesema itahakikisha inatenga bajeti  ya shilingi milioni 50 kuwezesha mafunzo na kuboresha sekta ya kilimo kutoka  kwenye fedha zake pamoja nakuwaomba  wadau wengine wa wilaya kama vileKampuni ya uchimbaji dhahabu ya geita GGM kuchangia milioni 200 ili kuinua sekta hiyo.
 
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa wilaya hiyo,  Herman Clement Kapufi wilayani humo  jana wakati akifungua mafunzo ya siku moja kwa maofisa ugani wote wa wilayani yake  yaliyoandaliwa na Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH),  yenye lengo  la kuwakumbusha wataalamu hao wa kilimo nafasi yao pamoja na kuwapatia mbinu mpya za kisasa katika kulima mazao ya Mihogo, Pamba na Viazi vitamu katika kuelekea serikali ya viwanda.
 
Mkuu huyo wa wilaya amesema kazi hiyo nzuri iliyoanzishwa na COSTECH kupitia  Jukwaa la Bioteknolojia nchini (OFAB) hazitakuwa na maana endapo mafunzo hayo  hayatasimamiwana halmashauri yake ili kuhakikisha yanakwenda kuleta mabadiliko na  mapinduzi kwenye kilimo kwa wakulima kwenye maeneo mbalimbali. 
 
Kapufi amemtaka mkurugenzi wa halmashauri kuhakikisha anaweka bajeti kugharamia  mafunzo ya aina hiyo kwa maofisa ugani na wakulima badala ya kuwaachia COSTECH 
kufanya kazi hiyo peke yao wakati wanufaika ni wananchi wa wilaya hiyo na hivyo  kuahidi kuzungumza na wawekezaji wenye migodi kuweka bajeti kusaidia kilimo kwenye  fedha mbalimbali zinazotolewa nao kwaajili ya maendeleo ya halmahauri.
Amesema anatambua kuna wakulima wengine hawapendi kubadilika pale wanapofikishiwa  utaalamu lakini amewataka maofisa ugani hao kuto kata tamaa na badala yake wawe na 
mashamba yao binafsi ya mfano ambayo yatalimwa kwa kutumia kilimo cha kisasa na  mbegu bora ili waone badala ya kuzungumza kwa nadharia kila siku.
 
Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya hiyo Ali Rajabu,  amewapongeza watafiti hao kutoka COSTECH,OFAB na Kituo cha utafiti wa Kilimo Ukiriguru cha Mwanza  kwa kusaidia kuwawezesha maofisa ugani hao kupata mbinu bora  zaidia za kukabiliana na changamoto za kilimo kwa wakulima kwa kutumia teknolojia  za kisasa na kuiomba Halmashauri kuwapa vitendea kazi maofisa ugani wanaofanya  vizuri kwenye kata zao.
 
Amesema maofisa ugani ndio injini ya kilimo maana ndio wenye jukumu la kuwasaidia  wakulima kulima kisasa na kuzalisha kwa tija ikizingatiwa kuwa bila chakula hakuna  mtu anayeweza kufanya kazi na njaa hivyo tunahitaji chakula ili kuweza kufikiria 
kufanya kazi zingine za kimaendeleo.
 
Ameiomba COSTECH kutoishia kwenye wilaya hii pekee bali mafunzo ya aina hiyo  yafanywe nchi nzima kwani uhitaji ni mkubwa kwenye kila wilaya ili kuwakumbusha  kazi wataalamu hao wa kilimo na pia kuwapa mbinu mpya za kutatua changamoto  zinazowakabili wakulima kwenye mazao hayo ya pamba mahindi, mihogo na viazi lishe
 
Amesema imefika wakati sasa wananchi wa mkoa huo kubadilika na kutofikiria dhahabu kila wakati badala yake wajishughulishe na shughuli za kilimo tena cha kisasa kwa kutumia fursa ya ziwa Victoria katika kulima kilimo cha umwagiliaji na hivyo kuongeza tija
Awali akizungumza kabla ya kumkaribisha Mkuu wa wilaya Mratibu wa Jukwaa la  Biotehnolojia kwa maendeleo ya kilimo nchini (OFAB)Philbert Nyinondi kwa niaba ya  COSTECH amesema lengo la mafunzo hayo ni kuwasaida wataalamu hao wa kilimo kupata  mbinu mpya za uzalishaji na kuwajengea uwezo kwenye kuzalisha mazao hayo muhimu  ambayo yana mchango mkubwa katika kusaidia kupata malighafi kwaajili ya viwanda.
 
Amesema mafunzo hayo baada ya kutolewa kwa maofisa ugani pia yatatolewa kwa  wakulima kwenye vikundi na kisha kuwapatia mbegu bora na safi za mihogo na viazi  lishe ili kuanzisha mashamba darasa kwenye vijiji vitakavyochaguliwa ili wakulima waweze kuona na kujifunza na kisha kuwa sehemu ya mbegu bora kwenye wilaya.
 
Nyinondi amesema mpango huu ni sehemu ya utekelezaji wa majukumu ya Tume ya Taifa  ya Sayansi na Teknolojia katika kuhakikisha sayansi,teknolojia na tefiti nzuri  zinawafikia walengwa na kuleta tija kwenye sekta husika ili kuongea tija.