Wiki ya Jinsia EAC kuanza Jumatatu Arusha

Logo ya Jumuiya ya Afrika Mashariki

Na Nicodemus Ikonko, EANA

SEKRETARIETI ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kwa kushirikiana na taasisi tatu tofauti imeaandaa ‘Wiki ya Jinsia’ itakayoanza Jumatatu ijayo, kuhamasisha jamii kuelewa umuhimu wa kuheshimu masuala ya jinsia, hususan ni haki za wanawake na wasichana.

Taasisi zilizoshirikiana na Sekretarieti kufanya maandalizi ya
maazimsiho hayo ni pamoja na Shirika la Kimataifa la Ushirikiano la Ujerumani (GIZ),Taasisi ya East African Sub-Regional Support Initiative (EASSI) na Manispaa ya Arusha.

Tukio hilo linaenda sambamba na maazimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wanawake Duniani Machi 8, na pia kuunganishwa na Kampeni ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ya Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake
(UNiTE) Machi 9, inaeleza taarifa iliyotolewa na Idara ya Mawasiliano na Uma ya EAC na Shirika Huru la Habari la Afrika Mashariki (EANA)
kupata nakala yake.

Naibu Katibu Mkuu wa EAC, anayeshugulikia Sekta za Uzalishaji na Jamii, Jean Claude Nsengiyumva anafafanua katika taarifa hiyo kwamba tukio hilo la wiki zima (Machi 5-9) litatoa mwanga kwa EAC kuona umuhimu wa kuweka mikakati ya sera zinazozingatia masuala ya jinsia.

“Hususan ni katika migogoro inayohusisha mapambano yanayotumia silaha, ukatili wenye misingi ya kijinsia ni uhalifu mkubwa, hatari kwa jamii na ni gharama kwa afya ya jamii. Raia, hususan wanawake na watoto, ndiyo wanaoathrika zaidi na mapambano ya silaha. Kwa mfano huishia kuwa wakimbizi na watu wasiokuwa na makazi ndani ya nchi zao,” anafafanua Nsengiyumva katika taarifa hiyo.

Anasisitiza kwamba; “Wote tunapaswa kufanya kila jitihada kuepuka vitendo vya kikatili kwa kuielimisha jamii na kwamba wiki hii ya kwanza ya Wiki ya Jinsia EAC,ndiyo jambo litakalofanyika.”

Mgeni rasmi katika tukio hilo ni Balozi Tegla Loroupe wa Kenya, mshindi mara mbili wa mbio ndefu za wanawake duniani.

Balozi Loroupe anafahamika sana katika kanda hii kwa juhudi zake za kupinga vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto. Pamoja na mambo mengine amefanikiwa kwa kiasi kikubwa kupunguza mapambano ya
kunyang’anyana ngo’mbe kwa kutumia silaha, Kaskazini mwa Kenya, Kusini mwa Sudan, Kaskazini-Mashariki mwa Uganda na Ethiopia.

Pia anasifiwa kwa kuleta amani katika maeneo hayo yenye migogoro na kumpatia tuzo mbalimbali za kikanda na kimataifa.

Naye Meneja Mipango ya Uhamasishaji Amani na Usalama wa GIZ, Miriam Heidtmann, anasema: “Usawa wa wanawake na wanaume ni sehemu ya utamaduni wa GIZ”, na kuongeza kwamba GIZ ina utamaduni wa muda mrefu
wa kuhusisha masuala ya jinsia katika shuguhuli zake na ina mikakati ya kuiboresha kila mara.

Anaeleza kwamba mikakati hiyo inaotokana na dhana kwamba maendeleo yanaweza kuwa endelevu tu iwapo wanawake na wanaume wanafaidika sawa kisiasa, kiuchumi, kijamii na maendeleo ya utamaduni na pia
wakizitumia vilivyo fursa walizonazo.

Miongoni mwa shughuli zitakazofanyika katika Wiki ya Jinsia ni pamoja na washa ya kuhamasisha wafanyakazi wa EAC juu ya namna ya kuingiza masuala ya jinsia katika mipango na shughuli zao itakayofanyika Machi 5 katika hoteli ya Snow Crest.

Shughuli nyingine zimepangwa tofauti katika Kituo cha Mikutano ya Kimataifa cha Arusha (AICC) na Bwalo la Maafisa wa Polisi, Arusha.
Shughuli hizo ni pamoja na washa mbalimbali, maonyesho ya picha, vipeperushi, video na vitabu.

Machi 8, ambayo ni Siku ya Kimataifa ya Wanawake Duniani, kutakuwapo maandamo yatakayoanzia katikati ya mji hadi kwenye Ukumbi wa Manispaa ya Arusha, ambako viongozi mbalimbali watatoa hotuba.

Machi 9, wajumbe watashiriki washa ya UNiTE itakayohusu Kampeni ya Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Wasichana.