WHO Yaipa Msaada wa Magari TFDA

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Bi. Regina Kikuli akionesha ufunguo wa gari wa moja ya magari saba yaliyotolewa leo ambapo ni msaada kutoka WHO na vifaa vingine vyenye thamani ya sh. bilioni 2.4 katika hafla iliyofanyika jijini Dar es Salaam. katika hafla iliyofanyika jijini Dar es Salaam. Katika msaada huo magari mengine 22 yatatolewa baade.PICHA NA MAGRETH KINABO – MAELEZO

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Bi. Regina Kikuli akijaribu kuwasha gari kati ya magari saba yaliyotolewa leo ambapo ni msaada kutoka WHO na vifaa vingine vyenye thamani ya sh. bilioni 2.4 katika hafla iliyofanyika jijini Dar es Salaam. katika hafla iliyofanyika jijini Dar es Salaam. Katika msaada huo magari mengine 22 yatatolewa baade.

Na Frank John – MAELEZO

SHIRIKA la Afya Duniani (WHO) limekabidhi msaada wa vifaa mbalimbali wenye thamani sh. bilioni 2.4 kwa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ili kusadia katika kupunguza vifo vya watoto wachanga walio chini ya miaka mitano na kuiwezesha Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) katika utendaji wake. Msaada huo umetolewa leo na Mwakilishi Mkazi wa WHO Dk. Rufaro Chatora, ambapo alimkabidhi Naibu Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Bi. Regina Kikuli katika hafla iliyofanyika jijini Dar es Salaam.

Akikabidhi msaada huo, Dk. Chatora amesema shirika hilo linathamini juhudi za serikali katika kupunguza vifo vya watoto ndio maana linaipongeza kwa kutimiza malengo ya milinea ambapo watoto wote wamefaidika na malengo hayo. Alivitaja baadhi ya vifaa hivyo kuwa ni majokofu 128, komputa nne magari saba ya aina mbalimbali mashine za kutolea kopi, vifaa vya kufuatilia ubaridi ndani ya majokofu yatakayotumika kutunza dawa kwa ajili ya chanjo za watoto walio chini ya miaka mitano, vifaa vingine kwa ajili ya kusaidia TFDA.

Akizungumzia kuhusu msaada huo, Bi Kikuli alibainisha kuwa umekuja kwa wakati muafaka ambapo serikali imekuwa ikishirikiana vyema na washirika wa maendeleo katika kutimiza malengo ya milenia hasa lengo la nne na tano ambayo yanalenga kuboresha sekta ya Afya kwa kupunguza vifo vya watoto walio chini ya miaka mitano kwa kuwapatia chanjo stahiki kwa wakati kwa kuwa chanjo ni haki ya kila mtoto.

Aliongeza kuwa serikali ya Tanzainia imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kutekeleza malengo ya milenia hasa lengo namba nne ambalo ni kupunguza vifo vya watoto walio chini ya miaka mitano, ambapo vifo hivyo vimepungua kutoka kutoka 147 kwa vizazi hai 1000 hadi 81 mwaka 1999 na vifo vya watoto chini ya mwaka mmoja kutoka 99 kwa vizazi hai 1000 hadi 51 katika kipindi cha mwaka 2010. Bi. Kikuli alitumia nafasi hiyo kwa niaba ya serikali kuwashukuru wadau wa maendeleo na chanjo na kuwahakikishikia kuwa msaada huo utatumika kwa makusudio yaliyopangwa ili kusaidia kuboresha afya za Watanzania hususan watoto.