Wenyeviti Serikali za Mitaa Wabanwa Juu ya Taarifa za Mapato na Matumizi ya fedha

Naibu Waziri wa TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora, Jafo Selemani Saidi.

Naibu Waziri wa TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora, Jafo Selemani Saidi.

Na Ismail Ngayonga, Maelezo-Dodoma

SERIKALI imewataka Mwenyekiti wa Serikali za Vijiji nchini kutangaza na kuweza wazi taarifa za mapato na matumizi ya fedha za miradi ya maendeleo katika kipindi cha kila baada ya miezi mitatu (3).

Hatua ya kutotangaza taarifa hizo itaondoa uhalali wa mikutano mikuu unaohitajika kuitishwa na Viongozi hao katika kipindi hicho, kama inavyoelekezwa katika sheria ya fedha ya mamlaka ya Serikali za Mitaa ya mwaka 1982.

Hayo yamesemwa leo mjini Dodoma na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), George Simbachawene wakati wa mahojiano yake na waandishi wa habari waliotaka kufahamu umuhimu wa wananchi wa vijijini kuifahamu bajeti ya Serikali.

Simbachawene aliwataka Viongozi waliopo katika mamlaka ya Serikali za Mitaa wakiwemo Madiwani kusimamia kikamilifu suala hilo ili kuhakikisha kuwa wananchi waliowachagua wanafahamu matumizi ya fedha mbalimbali zinazotumwa na Serikali katika Halmashauri za Wilaya.

“Wapo baadhi ya Wenyeviti wamekuwa wakificha taarifa hizo kutokana na maamuzi yasiyo ya busara katika matumizi ya rasilimali ikiwemo uuzaji wa ardhi, hatua inayopelekea migogoro ambayo kimsingi haina umuhimu wowote” alisema Simbachawene.

Kwa mujibu wa Simbachawene alisema Mwenyeviti wa Mitaa, Vijijini na Vitongoji hawana budi kutambua kuwa dhana ya ugatuaji wa madaraka kwa wananchi pamoja na mambo mengine inawahimizia viongozi hao kutoa taarifa hizo katika kipindi kilichowekwa kwa mujibu wa sheria.