Na Janeth Mushi, Arusha
MJUMBE wa Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) taifa na Mlezi wa CCM Mkoa wa Arusha, Stephen Wassira, amewataka wanachama wa chama hicho nchini kuwa askari wa Chama kwa kupambana na rushwa hasa wakati chama hicho kinapoelekea katika uchaguzi wake wa ndani.
Wassira ambaye pia ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Mahusiano, amesema hayo leo katika hafla ya maadhimisho ya miaka 35 ya kuzaliwa kwa CCM yaliyofanyika kimkoa katika viwanja vya Soko la Sombetini mjini hapa.
Amesema akiwa mlezi wa CCM Mkoa wa Arusha atahakikisha viongozi watakaopatikana katika uchaguzi wa viongozi kuanzia ngazi ya tawi hadi taifa wanakuwa waadilifu ndani na nje ya chama.
“Ili tuweze kufanikisha suala la kupata viongozi walio waadilifu, wanaojali maslahi ya wanachama wao na taifa kwa ujumla ni wajibu wa kila mwanachama kuwa TAKUKURU ya Chama na kupingana vikali na mbinu zisizo halali zaitakazotumika katika uchaguzi ikiwemo rushwa ambayo imekuwa adui mkubwa wa haki,” alisisitiza Waziri huyo
Aidha aliongeza kuwa chaguzi ambazo zinatarajiwa kufanyika
katika mkoa huu ikiwemo Uchaguzi wa Mbunge wa Jimbo la Arumeru
Mashariki kufuatia kifo cha aliyekuwa Mbunge wake Jeremiah Sumari(CCM) na uchaguzi katika kata ya Daraja Mbili kufuatia aliyekuwa diwani wa kata hiyo Bashiri msangi (CCM) kufariki dunia, Wasira alisema kuwa katika chaguzi hizo rushwa inatakiwa kuepukwa vikali ili kupata viongozi sahihi.
Hata hivyo aliwaomba viongozi wa chama mkoani hapa kushirikiana
na wanachama wake, kuwafuatilia kwa umakini wale watakaojitokeza
kuwania nafasi mbalimbali za uongozi na iwapo watagundua wanatoa
rushwa ili wapate madaraka, uongozi utoe taarifa ili waweze
kushughulikiwa.
Alisema kuwa iwapo itathibitika kweli walikiuwa wakitoa rushwa ili
kuchaguliwa, akiwa kama mlezi wa Chama hicho mkoa wa Arusha, atapeleka taarifa hizo katika vikao vya kamati kuu ili waweze kuondolewa katika kinyang’anyiro hicho kwa kukosa sifa za kugombea.
.
Akizungumzia baadhi ya vyama vya upinzani nchini, alibainisha kuwa
baadhi yao vimechangia kwa kiasi kikubwa kukwama kwa maendeleo
kutokana na sera mbovu ambazo zimekuwa zikiendeleza maandamano na migomo ambayo huwakwamisha wananchi kufanya kazi za maendeleo
Alisikitishwa kwake na baadhi ya wasomi wa vyuo vikuu na kudai kuwa
wamekuwa wepesi kudanganywa na wanasiasa wasio waadilifu ambao
wamekuwa wakijiona ni wasafi kuliko wa CCM ambapo amewata mara moja kuacha kuzungumza hovyo lasivyo atawaumbua mmoja baada ya mwingine kwani anafahami baadhi ya ambao ni mafisadi kuliko wale wa CCM wanaotuhimiwa ni mafisadi.
“Nashangazwa na wanasiasa hususani Wapinzani ambao wanajiona ni wasafi huku wakiwa wanajitambua kuwa si wasafi ni mafisadi, siogopo nitawataja wale wote kwani nian imani mnajua jina langu la kisiasa ni Tyson sasa, nawamezea kwa sasa ila wakijibu nitwaumbua wote,” alidai.
Maadhimisho hayo ya miaka 35 ya kuzaliwa kwa CCM toka chama kikongwe cha TANU yanafanyika kitaifa mkoani Mwanza ambapo yamepewa kauli mbiu isemayo CCM ya sasa italetwa na mimi mwenyewe.