Waziri wa Uchukuzi awalaumu Wabunge wa Upinzani

Waziri wa Uchukuzi, Omar Nundu

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

WAZIRI wa Uchukuzi, Omar Nundu amewatupia shutuma baadhi ya wabunge wa kambi ya upinzani bungeni akidai kuwa wameagizwa na kampuni binafsi kuupinga mswada wake bungeni.

Nundu alitoa kijembe hicho alipopata nafasi ya kuchagia upande wa Serikali kuwatoa wasiwasi baadhi ya wabunge juu ya mabadiliko katika sheria mpya kwenye Muswada wa Sheria ya Ununuzi wa Umma, uliyowasilishwa na Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkulo bungeni ukikusudia kufuta sheria ya ununuzi wa umma, sura 410 ya mwaka 2004 na kutunga sheria mpya ya mwaka 2011.
“Wengine hapa mnatumwa na wenye kampuni binafsi za ndege kubabaisha watu humu ndani ili serikali isiinuke, mnadhani hatujui kama baadhi yenu mnatumiwa,” alisema Waziri Nundo na kuwafanya wabunge wa upinzani kuchachamaa lakini Mwenyekiti wa Kikao, Goerge Simbachawene aliingilia kati.

Hata hivyo muswada huo umepitishwa leo licha ya kukabiliana na upinzani mkubwa kutoka kwa wabunge wa kambi ya upinzani waliokuwa wakipinga vifungu namba 65 na 66. Kile cha 65 (1) kinasema manunuzi ya dharura yanaweza kufanywa pale ofisa masuuli atakapojiridhisha kuwepo na maslahi ya umma, huku kile cha 66 (1) kikiruhusu serikali kufanya manunuzi ya vifaa maalum vilivyotumika kutokana na gharama yake kuwa kubwa.
Akifafanua zaidi Nundu alidai usafiri wa ndege si anasa kama baadhi ya wabunge walivyodai na nia ya Serikali kuwasilisha muswada huo ni jitihada za kuliwezesha Shirika la Ndege nchini (ATCL) kumiliki ndege nyingi ili wananchi wanufaike na huduma hiyo.