WAZIRI wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo amesababisha kuvunjika kwa kikao cha Bunge kilichokuwa kikiendelea usiku huu mjini Dodoma baada ya azimio la kumuwajibisha lililotolewa na Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kuleta mzozo katika kikao hicho kabla ya kuvunjika.
Bunge lilikuwa likipitia mapendekezo ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) iliyofanya uchunguzi wa tuhuma za uchotwaji wa takribani sh. bilioni 306 zinazodaiwa kuporwa benki kuu kupitia akaunti ya Tegeta Escrow na kupitisha moja moja kabla ya kikao hicho kuvunjika baada ya kufika katika pendekezo la kumwajibisha Prof. Muhongo.
Baada ya kusomwa kwa pendekezo hilo baadhi ya wabunge wakiwemo wapinzani walitaka Bunge limshauri Rais atengue uteuzi wa Profesa Muhongo kwa madai alishindwa kutekeleza majukumu yake na kusababisha uporwaji wa kiasi cha sh. bilioni 306 pamoja na kulidanganya bunge juu ya sakata hilo katika ufafanuzi wake.
Kwa upande wa serikali waliomba bunge lisipitishe azimio la kumtaka Rais atengue uteuzi wa Prof. Muhongo na badala yake kutaka lipitishwe azimio la kushauri uchunguzi ufanywe na vyombo husika juu ya kiongozi na kuangalia kama amehusika kisha baada ya kubainika ndipo hatua nyingine zichukuliwe jambo ambalo lilizua mzozo mkubwa kwa wabunge hasa wa upinzani.
Wabunge wa upinzani walisimama na kugoma kukaa huku wakipaza sauti; “…hatukubali, hatukubali huku ni kutetea Wizi Waziri huyu lazima awajibishwe kwa uzembe alioufanya…hatukubali…,” yalisikika maneno ya baadhi ya wabunge wa vyama vya upinzani huku wengi wao wakiwa wamesimama.
Spika wa Bunge Anne Makinda alijitahidi kuwatuliza wabunge na kuwaomba wasitoke bungeni ili waweze kubishana kwa hoja jambo ambalo liligonga mwamba na kuamua kusitisha kikao hicho cha bunge bila kufikia muafaka wa azimio lililokuwa likijadiliwa.
Muda mfupi kabla ya kuvunjika kwa kikao hicho Spika Makinda alitoa nafasi kwa Kiongozi Mkuu wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe ambaye alisema hawawezi kukubali Prof. Muhongo aachiwe wakati ripoti ya CAG na uchunguzi wa Kamati ya PAC zimeonesha kulikuwa na dosari kwenye Wizara yake ambayo ndiyo iliozaa sakata la escrow hivyo kusisitiza wao hawatakubali kuwa sehemu ya kuwalinda wezi Serikalini.
Kabla ya kumaliza zomeazomea zilianza kusikika kutoka kwa baadhi ya wabunge huku wa upinzani kunyanyuka vitini na kutishia kutoka bungeni kama hali hiyo ya mvutano itamlinda Prof. Muhongo jambo ambalo lilizua mvutano kelele bungeni kabla ya Spika kuamua kusitisha bunge hilo bila suluhu.