Waziri wa Kenya awapasha viongozi Tanzania

Washirikiwa Kongamano la Kimataifa la utumishi wa umma wakimsilikiliza Waziri Mkuu wa Tanzania Mizengo Pinda (hayupo) pichani wakati wa ufunguaji wa kongamano hilo jijini Dar es Salaam. (Picha na Tiganya Vincent, MAELEZO-Dar es Salaam)

Na Anicetus Mwesa

WAZIRI wa Nchi Huduma za Jamii wa Kenya, Dalmas Anyango amewataka viongozi wa umma kutojiona miungu watu, na hivyo kuwatumikia wananchi wanaowaongoza.

Amesema watumishi wa umma wanapaswa kutambua kuwa wana deni la kuwatumikia wananchi wao, na kwamba kama kuna mtumishi yeyote hayuko tayari kuwahudumia wananchi kwa kazi ambayo aliiomba ni bora sasa akajiengua mwenyewe katika ofisi aliyoko.

Anyango alitoa kauli hiyo jana wakati akichangia mada kwenye Kongamano la Kimataifa la Utumishi wa Umma linalofanyika kwenye Ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam.

Alisema viongozi wa Serikali na watumishi wengine wa umma wanatabia ya kuwaona raia kama mbumbumbu na hivyo kutowahudumia kama wanavyohitaji.

Pia aliwataka viongozi wa umma kutojiamria mambo muhimu yanayohusu mustakali wa taifa bila kuwashirikisha wananchi wanaowaongoza, na kwamba hiyo ndiyo imekuwa ikisababisha machafuko.

“Viongozi wa umma katika serikali za kiafrika mara nyingi wanatumia mabavu kufanya mambo nyeti yanayohusu mstakabali wa taifa. Kutokana na hali hiyo nchi nyingi zimekuwa zikijikuta katika machafuko.

…Mambo muhimu yanayohusu mstakali wa taifa hayastahili kuamriwa na watu wachache hivyo ni wakati muafaka sasa kubadirika kwa kuwashirikisha wananchi ambao kimsingi ndiyo wenye nchi.

…Mtu anapokwenda katika ofisi za umma kwa ajili ya kwenda kupata huduma zake za msingi anakutana na majibu yasiyoridhisha na ya kukatisha tama, kimsingi ni kwamba watumishi wa umma hawawatendei haki raia,” alisema Anyango.

Anyango pia alikemea vitendo vya rushwa vinavyofanywa katika ofisi za umma na kuongeza kuwa vitendo hivyo ni vikwazo vya Maendeleo ya nchi yoyote ile.

“Huu ni wakati wa Bara la Afrika kupigana vikali na vitendo vya rushwa katika ofisi za umma na katika chaguzi zetu zinazofanyika katika nchi husika kwani mtu anapoingia madarakani ama ofisini kwa njia ya rushwa kamwe hata kuwa na dira ya kuleta maendeleo,” alisema.

Anyango ambaye pia ni Mwenyekiti wa mikutano ya Pan African wa Mawaziri wa Utumishi wa Umma aliwataka viongozi wa nchi za kiafrika kuacha kulalamika kwamba viongozi waliowatangulia hawakuziinua nchi zao kiuchumi.

“Hakuna sababu ya kuanza kuwalaumu viongozi waliopita hivyo huu ni wakati wa kufanya kazi za kuendeleza nchi zetu kwa kupambana na vitendo vyote vya rushwa, yaliyopita yamepita tuanze upya sasa,” alisema.