WAZIRI WA AFYA NA USTAWI WA JAMII ATEMBELEA HOSPITALI YA MKOMAINDO-MASASI.

Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Dkt. Hadji Mponda akiwaangalia watoto waliozaliwa kabla ya siku katika chumba cha joto, katika hospitali ya mkomaindo ambapo watoto hao wana wiki mbili toka kuzaliwa na wanaendelea vizuri.

Mbunge wa jimbo la masasi Mh. Mariam Kassembe akimbeba mmoja wa vichanga hivyo anayeitwa Magid Hussein mwenye umri wa wiki mbili na siku tatu katika wodi hiyo.(Picha zote na Catherine Sungura-MOHSW)

Mganga Mkuu wa Wilaya ya Masasi Dkt. Ignas Mlowe akifafanua jambo kwa Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Dkt. Hadji Mponda hayuko pichani,alipotembelea ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Masasi,katikaki ni Mkuu wa Wilaya Mh.Nape Nnauye,kushoto ni Mbunge wa jimbo hilo Mh. Mariam Kassembe.


Watendaji wakuu wa halmashauri za wilaya wametakiwa kushirikiana ili kuboresha na kuimarisha huduma za afya nchini. Wito huo umetolewa jana na Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Dkt. Hadji Mponda alipofanya ziara ya kikazi katika wilaya ya masasi. Dkt. Mponda alisema ili huduma za afya ziimarike ni vyema watendaji hao kushirikiana kwa pamoja na bodi ya afya za halmashauri husika ili kuleta maendeleo katika sekta hiyo. “Unakuta baadhi za bodi katika halmashauri nyingi zimepitwa na wakati ama wajumbe wake wameteuliwa kwa kufahamiana hivyo kunazorotesha huduma za afya pamoja na matumizi mazuri za rasilimali za afya nchini”. Alisema wananchi wanao wajibu wa kusimamia na kujua thamani za huduma za afya katika wilaya zao. Akisoma taarifa ya wilaya katika idara ya afya mganga mkuu wa wilaya hiyo Dkt . Ignas Mlowe alisema huduma za afya ya uzazi na mtoto,wilaya yake bado inakabiliwa na idadi kubwa ya akina mama wanaojifungulia majumbani kwa wakunga wa jadi au kwa jamaa zao. Alitaja sababu kubwa inayochangia akina mama wengi kujifungulia majumbani ni pamoja na umbali toka jamii zilizopo hadi kituoni pamoja na uhaba wa watumishi hivyo husababisha vifo vingi vya wajawazito wakati wa kujifungua. Dkt. Mlowe alisema tarajio lao la wanawke kujifungulia kwenye vituo vya huduma za afya ni 12,312 ambapo waliojifungua vituoni ni 7,695 sawa na asilimia 62.5 na waliojifungua nyumbani ni wanawake 318 sawa na asilimia 25.8 kutoka vituo vya afya 39 kati ya vituo 45 vinavyotoa huduma za kujifungua zikiwemo hospitali 2,vituo vya afya 3 na zahanati 34.