Na Hassan Abbas
WAZIRI wa Fedha wa Liberia ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati Ndogo ya Mawaziri wa Afrika wanaoratibu Mpango wa Afrika Kujitathmini Kiutawala Bora (APRM), Amara Konneh amesisitiza kuwa Mpango huo unapaswa kusaidiwa ili kuwafikia wananchi wengi wa Afrika.
Waziri Konneh alitoa wito kwa Umoja wa Mataifa (UN) na Jumuiya za Kimataifa kwa ujumla kuisaidia APRM kwa lengo la kuhakikisha kuwa Mpango huo si tu unabaki kupongezwa bali uendelee kuwa na thamani kwa wananchi wa nchi husika.
Waziri huyo aliyasema hayo mjini New York, Marekani mbele ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Bw. Ban Ki Moon wakati wa mjadala wa Wiki ya Afrika na NEPAD uliomalizika mwishoni mwa wiki jijini humo.
Katika mada yake, Waziri Konneh alisema APRM ni Mpango wenye athari za moja kwa moja kwa wananchi wa Afrika kwa sababu kila nchi iliyojiunga inawapa fursa wananchi kushiriki na kusisitiza kuwa APRM “si klabu ya mazungumzo tu bali mchakato wenye vitendo.”
Tanzania ni miongoni mwa nchi 33 za Umoja wa Afrika zinazoshiriki katika Mpango wa APRM na tayari imekamilisha Ripoti ya kwanza iliyotathmini hali ya utawala bora nchini kwa kuwashirikisha wananchi sehemu mbalimbali na itazinduliwa hivi karibuni.
Akizungumza katika moja ya mikutano ya APRM Rais Jakaya Kikwete alipata kusisitiza kuwa Tanzania imejiunga na APRM kwa sababu inajiamini katika eneo la kuboresha utawala bora lakini pia iko tayari kufaidika na manufaa ya Mpango huu.
Hata hivyo akizungumzia miaka 10 tangu kuanzishwa kwa APRM, Waziri Konneh alisema hakikuwa kipindi rahisi kwa nchi mbalimbali zilizoanza kutekeleza Mpango huo, kulikuwa na changamoto nyingi lakini APRM imebaki kuwa taasisi imara ya Kiafrika.
“Ni Mpango wa Kiafrika uliobuniwa na Waafrika, unaoendeshwa na Waafrika ukiwa na lengo la kuingiza katika damu za watu wetu dhana ya kuheshimu demokrasia na utawala bora,” alisema Waziri Konneh.
Alitumia wasaa huo pia kuzipongeza nchi za Afrika zilizochukua uamuzi mgumu wa kujiunga na APRM ikiwemo kuruhusu wananchi wao waitathmini Serikali na nchi kwa ujumla kwa lengo la kubaini changamoto za pamoja na kuzifanyiakazi.
“Huku ni kudhihirisha wazi kuwa Afrika kwa sasa imeamua kukumbatia zaidi demokrasia na kuenzi misingi ya utawala bora ili kuimarisha misingi yetu ya utawala na maendeleo ya kijamii,” alisema.
Kati ya nchi 33 zilizojiunga kati ya 54 za Umoja wa Afrika, Tanzania ni miongoni mwa nchi 17 zilizokamilisha Ripoti ya kujitathmini kwa kuwapa nafasi wananchi na wataalamu kubaini mambo mazuri ya kuendelezwa na changamoto za kufanyiwakazi.