Na EleuteriMangi-MAELEZO
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) George Simbachawene amewaagiza wadau wa mradi wa mabasi yaendayo haraka yanayosimamiwa na Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART) kuhakikisha wanampatia taarifa ifikapo Aprili 3, 2016 ni lini mradi huo utaanza kutoa huduma.
Uamuzi huo wa Waziri Simbachawene unafuatia makubaliano yaliyofikiwa wakati wa kikao na wadau hao Machi 31, 2016 kilichofanyika ofisi za DART jijini Dar es salaam ili kuhakikisha wanatoa huduma ya usafiri wa uhakika kwa Watanzania na hasa wakazi wa jiji hilo.
“Kama mambo yote yataenda vizuri mradi huu utaanza mapema angalau mabasi 50 yaanze kutoa huduma mapema iwezekanavyo” alisema Simbachawene.
Simbachawene alisema kuwa hadi sasa mabasi mawili yamesha anza kufanya majaribio katika barabara za mradi huo na kuwahimiza wadau hao waongeze idadi ya mabasi yanayofanya majaribio angalau yafike 15 ili madereva wazoee barabara kabla ya mradi kuanza kutoa huduma rasmi.
Ili kuongeza kasi ya kukamilisha mradi huo, Simachawene amewataka wadau hao wa mradi wa mabasi yaendayo haraka wawe na utaratibu wa kukutana kila siku kwa kuzingatia kazi walizojipangia na kuangalia utekelezaji wake umefikia wapi na kumpatia taarifa kila baada ya siku mbili.
Aidha, Simbachawene amewaasa wa kazi wa jiji la Dar es salaam wawe watulivu kwa kuwa kazi kubwa ya mradi huo imekamilika na mradi umekaribia kuanza kuleta matunda na hivyo waitunze miundombinu hiyo ikiwemo barabara na vifaa vitakavyokuwa vinatumika wakati wa kutoa huduma.
“Kuhujumu miundombinu ya DART ni kulihujumu taifa letu, watu wote ni lazima wawe na uzalendo kwa mali yao ili mradi uwe wa tija kwa manufaa ya nchi yetu” alisema Simbachawene.
Simbachawene amesema kuwa utunzaji wa miundombinu hiyo utafanikiwa iwapo kutakuwa na ushirikiano mzuri kati ya wananchi, wadau wa mradi wa DART na Serikali.
Katika kikao hicho na wadau wa mradi wa DART, Waziri Simbachawene aliambatana na Naibu Waziri wake Selemani Jaffo pamoja na viongozi mbalimbali wa Serikali.
Mabasi ya Mradi wa Mabasi yaendayo haraka yatakuwa yanafanya safari zake ya kutoa huduma ya usafiri kwa wananchi kupitia eneo la Kimara, Ubungo, Morocco, Magomeni, Feri na Kariaakoo.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Takwimu UDART Hamdi Al-Hadj amesema kuwa kutakuwa na jumla ya mabasi 140 ambayo yanatarajiwa kutoa huduma katika mradi wa DART jijini Dar es Salaam.
Kikao cha Waziri Simbachawene kilihuwahusisha wadau wa mradi huo ambao ni DART, TANROAD, Msajili wa Hazina, Kampuni ya Simon Group, SUMARTA, Wakala ya Serikali Mtandao (eGA) na Jeshi la Polisi.