WAZIRI wa Ujenzi Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa ametoa mwezi mmoja kwa kampuni za simu nchini zilizoingia makubaliano na Serikali kupeleka huduma ya mawasiliano vijijini kukamilisha kazi hiyo vinginevyo hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.
Prof. MBARAWA ametoa agizo hilo mkoani IRINGA mara baada ya kukagua mitambo ya kampuni ya simu ya TTCL na kubaini kwamba bado kuna baadhi ya vijiji havijafikiwa huduma ya mawasiliano licha ya mkataba wa kutekeleza kazi hiyo kati ya Serikali na kampuni hizo kusainiwa miaka miwili iliyopita.
“Tulikubaliana kwenye mkataba na tukawapa fedha kwa ajili ya kupeleka mawasiliano vijijijni hivyo ifikapo mwezi julai kampuni yoyote ya simu itakayokuwa haijatimiza makubaliano hayo tutaipiga faini,” Alisema Prof. MABARAWA.
Kuhusu suala la kukatwa kwa mkongo wa taifa wa mawasiliano katika baadhi ya maeneo ya Mkoa wa IRINGA Prof. MABAWA alisema hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa mtu au taasisi itakaye haribu miundombinu hiyo.
Aidha, amemuagiza meneja wa TTCL mkoa wa Iringa Eng. Ekael Manase kuhakikisha kuwa minara iliyojengwa katika maeneo ya vijiji Mkoani humo inaanza kutoa huduma ya mawasiliano kabla ya mwisho wa mwezi huu.
Katika hatua nyingine Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa amekagua barabara ya Iringa-Kalenga hadi Hifadhi ya Taifa ya Ruaha yenye urefu wa KM 134 ambayo usanifu wake umekamilikka na kusisitiza kuwa itajengwa kwa kiwango cha Lami.
Naye Mbunge wa Isimani ambaye ni Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Willium Lukuvi amesema ujenzi wa barabara hiyo ukikamilika utafufua uchumi wa Mkoa wa Iringa kwa kuwa utavutia wawekezaji na watalii katika Hifadhi ya Ruaha.
Prof. Mbarawa yuko katika ziara ya siku nne katika Mkoa wa Iringa ya kukagua maendeleo ya Miundombinu ikiwa ni mkakati wa Serikali kufufua uchumi wa Mkoa huo.