Waziri Pinda: Tafuteni Njia ya Kuinusuru MSD

WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amemwagiza Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Seif Rashid awasiliane na Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) ili watafute njia ya kuinusuru Bohari ya Dawa (MSD).


 
WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amemwagiza Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Seif Rashid awasiliane na Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) ili watafute njia ya kuinusuru Bohari ya Dawa (MSD).
 
Amesema hawana budi kutafuta njia ya kuhakikisha kuwa asilimia 67 inayotengwa na Mfuko wa Bima ya Afya (NHIF) kwa ajili ya kulipia dawa za wagonjwa mbalimbali inatumiwa ipasavyo na si vinginevyo.
 
Ametoa kauli hiyo leo mchana (Jumapili, Mei 5, 2013) wakati akizindua ghala jipya la kisasa la kuhifadhia dawa lililojengwa na Bohari ya Dawa, Kanda ya Dodoma  huko Kizota, nje kidogo ya mji wa Dodoma.
 
Ujenzi wa ghala hilo ambao umegharimu sh. bilioni 9.9/-, umechangiwa na Serikali ya Marekani kupitia Shirika lake la USAID na Mfuko wa Kimataifa wa Kupambana na UKIMWI, Kifua Kikuu na Malaria (Global Fund).
 
“Naibu Waziri kaeni na TAMISEMI ili itafute njia inayofaa kuzibana Halmashauri zote ili fedha inayotolewa na Mfuko wa Bima ya Afya zote ziende kutumika kwenye manunuzi ya dawa na si vinginevyo. Bima ya Afya wanataka asilimia 67 ya fedha wanayotoa itumike kulipa dawa na asilimia 33 iwe kwa matumizi mengine,” alisema.
 
Alikuwa kijibu risala ya MSD iliyosema Bohari ya Dawa inaidai Serikali kiasi cha sh. bilioni 52 ambazo zimelimbikizwa kutokana na madeni ya muda mrefu ya huduma za dawa, vifaa, na vifaa tiba ambavyo taasisi hiyo ilitoa kwa vituoa vya afya vya Serikali pamoja na hospitali zake.
 
Aliipongeza MSD kwamba licha ya mzigo mkubwa wa deni ilionao, haijaacha Kutoa huduma ya kununua na kusambaza kwa wananchi. Alisema Serikali itajitahidi kutafuta mbinu za kupunguza deni hilo katika bajeti ya mwaka huu.
 
Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na hadahara iliyohudhuria uzinduzi huo, Dk. Seif Rashid alisema hivi sasa Bohari ya Dawa ilikuwa inakodisha mita za mraba 24,000 kwa ajili kupata nafasi ya kuhifadhia dawa zinaingizwa kutoka nje ya nchi na kwamba kukamilika kwa ujenzi wa ghala hilo, lenye mita za mraba 5,310 kutasadia kupunguza gharama hizo.
 
Naye Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bohari ya Dawa, Bw. Cosmas Mwaifwani alisema kuanzishwa kwa taasisi kumesaidia kuongeza kiwango cha upatikanaji wa dawa kutoka asilimia 44 mwaka 1994 na kufikia asilimia 70 hadi 75 hivi sasa.
 
Alisema ili kuhakikisha dawa zinapatikana kwa wakati hadi vijijini, Bohari ya Dawa imeshaingiza mikoa 10 kwenye mfumo wake wa usambazaji wa dawa moja kwa moja hadi kwenye vituo vya afya badala ya kuishia kwa Mganga Mkuu wa Wilaya.
 
Alisifu Halmashauri sita na hospitali moja ya mkoa kwa kuwa mfano bora kwenye usimamizi na matumizi ya dawa zinazotolewa na kusambaza na Bohari ya Dawa. Alizitaja Halmashauri hizo kuwa ni Iramba, Bariadi, Igunga, Chamwino, Bahi na Sumbawanga. Aliitaja Hospitali ya Mkoa wa Iringa kuwa ndiyo iliyofanya vizuri kuliko hospitali nyingine nchini.
 
Uzinduzi huo ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa mkoa wa Dodoma, mwakilishi wa wahisani, wafanyakazi wa MSD na wakazi wa Kizota.