Waziri Pinda azindua kiwanda cha Bia ya Serengeti

Waziri Mkuu wa Tanzania, Mizengo Pinda (wa pili kushoto) akizungumza na mmoja wa Waziri wa Kenya (wa pili kulia) na viongozi wa juu wa SBL mara baada ya kuzindua rasmi kiwanda cha bia cha kampuni hiyo.

Na Joachim Mushi, Kilimanjaro

WAZIRI Mkuu wa Tanzania, Mizengo Pinda amesema Serikali inatambua mchango mkubwa wa huduma kwa jamii unaotolewa na kampuni ya Bia ya Serengeti Breweries (SBL), kupitia kitengo chake maalumu cha kuwahudumia wananchi (CSR).

Pinda alisema takwimu zinaonesha SBL kwa mwaka 2010, mbali na kulipa kodi ya bilioni 35.8, imetumia sh. milioni 350 kuwapatia maji safi na salama wananchi zaidi ya 270,000, pia SBL imechangia kiasi cha bilioni 2 kwenye elimu na kutumia sh. milioni 500 kwa ajili ya kuwasomesha wanafunzi wenye vipaji maalumu.

Waziri Pinda ametoa taarifa hiyo leo mjini hapa alipokuwa akizindua rasmi kiwanda kipya kikubwa cha Bia ya Serengeti kilichojengwa eneo la Boma Mbuzi, mkoani Kilimanjaro.

Alisema kujengwa kwa kiwanda hicho mkoani Kilimanjaro ni mtaji mkubwa wa ukuaji wa uchumi wa mkoa na Taifa kwa ujumla, hivyo kuwashauri wananchi kutoa ushirikiano katika kuanga mkono juhudi ya kukiendeleza kiwanda hicho.

Waziri Mkuu wa Tanzania, Mizengo Pinda (wa pili) akipata ufafanuzi kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji EABL, Seni Adetu (wa pili kulia) wengine ni viongozi mbalimbali waliohudhuria uzinduzi huo.


Kukamilika kwa kiwanda hicho ambacho kwa sasa kimeajiri wafanyakazi wa kudumu na muda mrefu 400 na wengine 1000 kwa ajira anuai zilizochangia na uwepo wa kiwanda hicho; kutasaidia kukua kwa kasi kwa uchumi wa Mkoa wa Kilimanjaro ambao ulianza kulega lega kutokana na kufa kwa viwanda kadhaa hapo awali.

Alisema kiwanda cha Serengeti kupitia bia yake maarufu ya Serengeti imekuwa ikilitangaza jina la Tanzania nje ya mipaka ya nchi, hivyo kufarijika na uwamuzi wa viongozi wazalendo wa SBL kuamua kuuza hisa- zaidi ya wazo la kukiuza kiwanda choche jambo ambalo lingeweza kupoteza jina hilo la kizalendo.

“Serikali inatambua ufanisi ambao Kampuni ya Bia ya Serengeti imekuwa ikionesha katika kuhakikisha kuwa inaimarisha biashara zake na kuweka misingi imara ya maadili ya kibiashara pamoja na yale ya kiutu katika shughuli zake. Misaada na uwekezaji katika masuala ya kijamii ni mambo ambayo yana thamani kubwa…,” alisema Waziri Pinda.

Aidha Pinda alisema kukua kwa sekta ya viwanda nchini Tanzania ndiyo njia pekee ya kuleta maendeleo ya haraka nchini. “Ukuaji wa sekta ya viwanda unakwenda sambamba na kukua kwa kasi kwa sekta nyingine anuai,” alisema Waziri Mkuu akitoa hotuba yake.

Aliongeza kuwa kuna haja ya Watanzania hasa wakulima kutumia fursa ya kulima maligafi ya mtama mweupe ambao unatumiwa pia na kiwanda hicho katika uzalishaji wake, hatua ambayo inaweza kuwaongezea kipato zaidi ya mazao mengine.

Akizungumza awali Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Kiwanda hicho, Jaji Mstaafu, Mark Momani alisema SBL imewekeza zaidi ya bilioni 12 kwenye kiwanda hicho, hivyo kinauwezo wa kuzalisha vinywaji vya kutosha nchini pamoja na mataifa mengine ya jirani kama Kenya, Uganda, Rwanda na hata Congo (DRC).

Bomani aliutaka uongozi wa kiwanda hicho kuandaa utaratibu ambao utawashirikisha wakazi wa mjini Moshi kukitembelea kiwanda hicho ili nao waweze kutoa maoni na ushauri ambao unaweza kuboresha zaidi kiwanda na kuleta mafanikio kwa wote.

Alisemara nia ya SBL ni kujenga kiwanda bora ambacho kinaweza kuleta mabadiliko kwa wananchi na taifa kwa ujumla. Awali Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Leonidas Gama akizungumza kabla ya kumkaribisha Pinda, alisema kujengwa kwa kiwanda hicho ni mafanikio ya wakazi wa Moshi kwani watapata fursa mbalimbali hivyo kukuza kipato.

“Tunajua kuna ajira nyingi zimeletwa na kiwanda hiki, ule wa moja kwa moja na mwingine unaosababishwa na shughuli anuai za uwepo wa kiwanda hiki,” alisema Gamba ambaye aliwataka wawekezaji zaidi kwenda Kilimanjaro kufanya shughuli hizo.

Uzinduzi wa kiwanda hicho uliohudhuriwa na viongozi mbalimbali wa vyama na Serikali, wafanyabiashara wakubwa, wageni waalikwa wakiwemo wahariri kutoka vyombo mbalimbali vya habari pamoja na wazee wa jadi.