Waziri Pinda Ataka Busara Kumaliza Mgogoro Kagera, Alia na Madawati…!

Naibu Waziri wa TAMISEMI, Agrey Mwanri (kulia) na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh (kushoto) wakiteta jambo na Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Fabian Massawe (kati) kushughulikia mgogoro huo hivi karibuni.

Naibu Waziri wa TAMISEMI, Agrey Mwanri (kulia) na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh (kushoto) wakiteta jambo na Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Fabian Massawe (kati) kushughulikia mgogoro huo hivi karibuni.


 
Na Mwandishi Wetu, Kagera

WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda ameutaka uongozi wa mkoa wa Kagera ukae na kuzungumza ili kutafuta ufumbuzi wa mgogoro wa kisiasa katika Manispaa ya Bukoba kwa manufaa ya wananchi. Ametoa wito huo Oktoba 5, 2014 wakati akizungumza na viongozi na watendaji wa Serikali wa mkoa huo mara baada ya kupokea taarifa ya mkoa huo iliyowasilishwa kwake na Mkuu wa Mkoa huo, Kanali (Mst) Fabian Massawe.
 
Waziri Mkuu aliwasili Bukoba jana jioni akitokea Dodoma ili kumwakilisha Rais Jakaya Kikwete kwenye maadhimisho ya Siku ya Walimu Duniani ambayo kitaifa yanafanyika mkoani Kagera.
 
Waziri Mkuu Pinda alisema: “Ninatumaini viongozi mtakaa na kuzungumza na kukubaliana kuondoa kesi mahakamani ili kazi za kusaidia wananchi zifanyike…. Wewe kiongozi si kitu chochote, wenye kustahili kupewa uzito ni wananchi,” alisema.
 
Alisema anaumizwa na viongozi wa mkoa huo kukosa uchungu kwa kuwanyima wakazi wa manispaa hiyo uwezo wa kupata maendeleo kwa ajili ya mtu mmoja.
 
“Kuna hela zimetolewa na Benki ya Dunia kiasi cha sh. bilioni 18/- lakini zitapotea hivi hivi kwa sababu ya maslahi binafsi ya watu wachache. Pesa za maendeleo zinatakiwa zifanyiwe maamuzi katika vikao, lakini watu hawawezi kukutana sababu ya mtu mmoja.”
 
“Kuna fedha za maendeleo zinazotolewa na Serikali na ili zitumike ni lazima zipitishwe kwenye vikao lakini bila kujali maslahi mapana ya watu mtu anaenda mahakamani na kuzuia kila kitu kisifanyike hadi matakwa yake yatimizwe.”
 
Mapema, akiwasilisha taarifa ya mkoa, Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Kanali (Mst) Fabian Massawe alimweleza Waziri Mkuu kwamba tatizo la kisiasa katika Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba bado linaendelea.
 
Mkuu huyo wa mkoa alisema hivi sasa kuna zuio la mahakama (court injuction) la kutofanyika kwa vikao katika halmashauri lilitolewa Agosti 25, 2014 hadi hapo kesi namba 2/2014 iliyopo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Bukoba itakapohitimishwa. Alisema kesi nyingine mbili bado zinaendelea mahakamani baada ya kesi ya kutaka madiwani sita wavuliwe udiwani kutolewa hukumu mnamo Juni 25, 2014.
 
“Kuna kesi ya rufaa namba 11/2014 katika Mahakama Kuu ya Tanzania – Bukoba ya Mhe. Yusufu G. Ngaiza na wenzake watano dhidi ya Chifu Adronicius Kalumuna na Mkurugenzi wa Manispaa ya Bukoba, wakipinga uamuzi wa kuondolewa udiwani. Rufaa hiyo ilipokelewa Julai 18, 2014 na imepangwa kusikilizwa tarehe 13 Oktoba, 2014,” alisema.
 
Kesi ya pili ni kesi namba 02/2014 iliyopo Mahakama ya hakimu Mkazi Bukoba ya Mhe. Anatory Amani ya kutaka Mkurugenzi wa Manispaa amtambue kuwa yeye ni Meya wa Manispaa hiyo na kumpatia haki na stahiki zake. Kesi hii ilifunguliwa Agosti 12, 2014 na imepangwa kuanza kusikilizwa Oktoba 6, mwaka huu.”
 
Alimweleza Waziri Mkuu kwamba kulikuwa na kesi nyingine namba 01/2014 katika Mahakama Kuu ya Mhe. Anatory Amani dhidi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali na mwanahseria Mkuu wa Serikali ambayo ilifunguliwa Machi 7, mwaka huu ambapo mlalamikaji alitaka mambo kadhaa kuhusiana na taarifa ya ukaguzi maalum iliyotolewa Januari 17, 2014 yatenguliwe na mahakama.
 
“Aliiomba mahakama itengue taarifa hiyo kuwa batili na isitambulike kisheria lakini mahakama imeiondoa kesi hiyo tarehe 25 Septemba, 2014 kwa kuwa ilipelekwa mahakamani hapo chini ya kifungu kisicho sahihi,” alisema.

Wakati huo huo, Pinda ameutaka uongozi wa mkoa wa Kagera ulichukulie suala la upungufu wa madawati kwa uzito ule ule kama ilivyo kwenye suala la ujenzi wa maabara katika shule za sekondari.
 
Ametoa wito huo Oktoba 5, 2014 wakati akizungumza na viongozi na watendaji wa Serikali wa mkoa huo mara baada ya kupokea taarifa ya mkoa huo iliyowasilishwa kwake na Mkuu wa Mkoa huo, Kanali (Mst) Fabian Massawe.
 
Waziri Mkuu aliwasili Bukoba jana jioni akitokea Dodoma ili kumwakilisha Rais Jakaya Kikwete kwenye maadhimisho ya Siku ya Walimu Duniani ambayo kitaifa yanafanyika mkoani Kagera.
 
“Kwenye ujenzi wa maabara naona mnafanya vizuri lakini nataka kwa uzito uleule tusimamie suala la upungufu wa madawati. Tuunganishe nguvu za wananchi wa kawaida na za Serikali za Mitaa ili kuondoa kabisa tatizo hili mkoani mwenu,” alisema.
 
“RC hapa kasema kuna kata moja huko Bugandika kuna maprofesa 40. Huwezi kuwa na Maprofesa wote hao halafu kwenye shule wanakotoka maprofesa hao eti watoto wanakaa chini, haiwezekani!” alisisitiza.
 
Kwa mujibu wa taarifa kutoka ofisi ya Katibu Tawala wa mkoa huo, mkoa wa Kagera unahitaji madawati 238,080 kwa shule zote za msingi ambapo yaliyopo ni 138,876 na upungufu ni madawati 99,204. Kwa shule za sekondari, mkoa unahitaji viti 84,344, vilivyopo ni 82,275 na pungufu ni 2,069 wakati mahitaji ya meza ni 84,344; zilizopo ni 73,615 na upungufu ni 10,729.  
 
Aliwataka viongozi wa mkoa huo watafute mbinu za kukuza kipato cha wananchi wanaowaongoza kama njia mojawapo ya kuwasaidia wananchi wao kujikwamua kiuchumi. “Kwanza jiulize pato la mkoa likoje na limeongezeka kiasi gani? Je hali ya watu wangu ikoje? Nifanye nini ili niweze kuwaondoa hapo walipo na kuwafikisha katika kiwango kingine cha maendeleo?” alisisitiza.
 
Alisema kama kila kiongozi atadhamiria kupambana na umaskini wa kipato wa wananchi, ni dhahiri kuwa kazi ya kuondoa maadui wengine ambao ni maradhi na ujinga itakuwa rahisi mno.
 
Mapema, akiwasilisha taarifa ya mkoa, Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Kanali (Mst) Fabian Massawe alisema mkoa huo unahitaji kujenga maabara 570 ambapo zilizopo ni 136 wakati zingine 434 ziko katika hatua mbalimbali za ujenzi. Alisema mkoa unatumia maabara zinazohamishika (mobile labs) ambazo zipo 35. Aliosema mkoa huo pia unazo hosteli za wananfunzi 84 na unahitaji kujenga hosteli nyingine 212 ili kuwasaidia watoto wa kike waweze kuhitimu masomo yao.
 
Akizungumzia hali ya ulinzi na usalama mkoani humo, Kanali Massawe alisema kati ya Desemba 2013 na Septemba 2014, jumla ya wahamiaji haramu 1,589 kutoka nchi jirani za Burundi, Rwanda Uganda na DRC wameondoshwa nchini na wengine 231 waliondoka kwa hiari ikiwa ni utekelezaji wa Operesheni Kimbunga Endelevu.
 
“Katika operesheni Kimbunga ya awali wahamiaji 25,258 waliondolewa nchini ikiwa ni sawa na asilimia 48 ya wahamiaji wote 50,520 wanaokadiriwa kuwepo mkoani Kagera. Tangu wakati huo, tumeendelea na misako kwenye mabasi, maeneo ya starehe, nyumba za kulala wageni, viwandani, mashambani, taasisi za elimu, taasisi za madhehebu ya kidini, vipenyo na vijiji vya mpakani.”
 
“Kuanzia Januari hadi Septemba mwaka huu, jumla ya watu 572 walikamatwa na kufikishwa mahakamani au kufukuzwa nchini (PI). Walioshtakiwa walikuwa ni 431 na kuhukumiwa vifungo ama kutozwa faini na wahamiaji 231 walifukuzwa nchini kwa PI,” alifafanua.