Waziri Pinda Aendesha Harambee kuchangia visima Tisa

WAZIRI MKUU Mizengo Pinda ameendesha harambee ya papo hapo na kufanikiwa kuchangisha sh. milioni nane kwa ajili ya ukarabati wa pampu za visima tisa vya maji kwa wakazi wa kijiji cha Magamba, kata ya Magamba wilaya ya Mlele mkoani Katavi.

Waziri Mkuu alilazimika kuendesha harambee hiyo jana mchana (Jumapili, Januari 6, 2013) wakati akijibu hoja za wakazi wa kata hiyo kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa shule ya sekondari Magamba wilayani Mlele.

Kaimu Mhandisi wa Maji wa Wilaya hiyo, Bw. Enock Msengi alisema wanakijiji hao kupitia kamati ya maji walikuwa na sh. 150, 000/- kwenye akaunti yao. “Kama wangekuwa na fedha walau sh. milioni tatu, tungemudu baadhi ya gharama, lakini kwa hizi fedha alizochangisha Waziri Mkuu, tunaweza kukarabati visima vyote na vikafanya kazi… vinavyohitajika zaidi ni vipuri vya pampu,” alisema mara baada ya mkutano huo.

Akizungumza na wakazi hao, Waziri Mkuu aliwasisitiza watumie kilimo cha sesa ili kiwe mkombozi wao. Alipowaita mbele ya hadhara mabalozi wa mashina 18 na kuhoji kila mmoja wao analima ekari ngapi na anatumia kilimo gani, alibaini kuwa ni balozi mmoja tu ambaye anatumia kilimo cha sesa na amepanda kwa mistari na kutumia mbolea.

“Hawa wana ekari moja hadi ekari tano lakini wengi wao mmesikia ni matuta, matuta, matuta hata kwenye karanga wametumia matuta. Nawasihi sana mwakani kila mmoja atumie kilimo cha sesa kwa sababu kina tija zaidi kuliko hayo matuta… yanapoteza sehemu kubwa ya ardhi ya kilimo,” alisisitiza.

Waziri Mkuu ambaye alikuwa anamalizia ziara yake ya jimbo kwenye kata mbili kati ya 14 zilizobakia wakati wa ziara yake Desemba mwaka jana, aliwasihi mabalozi hao watumie umoja wa kikundi chao cha kilimo kuelimishana na akaahidi kuwatafutia majembe ya kukokotwa na ng’ombe ikiwa ni pamoja na kuwanunulia maksai ili waboreshe kilimo na wawe viongozi wa mfano.

Alipouliza kuna wafuga nyuki wangapi kwenye mkutano huo, walijitokeza wanane ambao jumla yao walikuwa na mizinga ya asili 34. Yeye aliahidi kuwapatia mizinga 50 ya kisasa (ya vibao na ya ngazi) ili waboreshe ufugaji wao.

Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo pia kuhimiza ujasiriamali kwa kuwaunga mkono akinamama wa Magamba ambao wanauza matunda na kuahidi kuwapatia sh. milioni tano ili ziwasaidie kuboresha biashara zao lakini akawataka waunde umoja, wachague viongozi na kuchangishana fedha za kianzio.

“Hapa Magamba siyo mbali na Mpanda mjini ambako yako Makao Makuu ya Mkoa… ninyi mnaweza kuwa chanzo kizuri cha kuwalisha wale watu wa mjini matunda na mbogamboga kwa sababu ya mabonde mliyonayo, tumieni hiyo fursa vizuri,” aliwasisitizia.

Mapema, Waziri Mkuu alikagua shamba la miembe ya kisasa la shule ya sekondari Magamba na kuahidi kuwaongezea miche mingine 100. Wakati linaanzishwa Desemba 15, 2010, shamba hilo lilikuwa na miche 80 lakini 11 imekufa na imebakia 69. Wanatarajia kuanza kuvuna maembe ya kwanza Desemba, mwaka huu.