*Atilia shaka takwimu za vocha za pembejeo
Na Mwandishi Maalumu
WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda ameonesha wasiwasi juu ya takwimu za matumizi ya vocha za pembejeo mkoani Mara hatua iliyomfanya atoe agizo la kuwepo kwa daftari la mkulima kwani ndilo litawawezesha kupata takwimu zenye usahihi.
Hayo yalisemwa na Waziri Mkuu Pinda jana, Septemba 16, 2011 wakati akizungumza na viongozi wa Mkoa wa Mara muda mfupi baada ya kuwasili mkoani humo kwa ziara ya kikazi. Waziri Mkuu alionesha kutilia shaka takwimu hizo baada ya kusomewa taarifa ya mkoa ambayo ilionesha vocha mkoani humo zimetumika ipasavyo na zimewanufaisha walengwa.
“Kwa mujibu wa taarifa yenu, mna jitihada kubwa katika eneo la vocha lakini sitaki kuamini hizi takwimu hata kidogo kwa kuwa eneo hili lina wizi mkubwa na limejaa wajanja hivyo sidhani kama na nyie hamhusiki katika hili, msimu ujao hakikisheni mnafuatilia kwa ukaribu ili kubaini kama kweli walengwa wananufaika na hizo vocha,” alisema.
Alisema kuwa ili takwimu hizo ziwe za kweli ni lazima kila wilaya na mkoa kuwa na daftari la wakulima kwa kuwa litaonesha kila mkulima kalima zao gani na ukubwa wa eneo lake lakini pia itaonesha hata matumizi yake ya pembejeo. Alisema kuwa eneo la Vocha limekuwa moja ya maeneo yanayochakachuliwa kwa kiwango kikubwa hatua iliyoifanya Serikali kumwagiza Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kufanyia ukaguzi eneo hilo.
Akizungumzia kuhusu kilimo katika mkoa huo, Waziri Mkuu alisema kuwa bado hakina tija ya kutosha na ndio sababu kubwa iliyomfanya awe na mashaka na takwimu za vocha. Aliwataka viongozi kuhakikisha wanawahamasisha wananchi kwenye matumizi ya zana bora za kilimo na akasisitiza matumizi ya wanyama katika kilimo ili kiwe na tija inayotakiwa.
“Kila siku nasisitiza matumizi ya matrekta madogo kwa kuwa hilo ndilo jembe la mkulima lakini kinachoonekana hapa matumizi yake ndiyo yanakosewa hivyo hakikisheni kama mkoa mnakuwa na wataalam ambao watatoa mafunzo kwa wakulima kabla ya kuanza kuyatumia ili waweze kuyatumia na hatimaye waone matunda yake,” alisisitiza.
Kutokana na hali hiyo, aliwataka Wakurugenzi wa Halmashauri zote kuwa wabunifu katika kuwasaidia wananchi wao ili watoke hapo walipo.
Akizungumzia kuhusu ufugaji, aliwataka waangalie uwezekano wa kupunguza idadi ya mifugo iliyomo mkoani humo ili iendane na eneo la malisho ya mifugo yao.
Aidha, aliwataka pia waangalie uwezekano wa kuweka jitihada katika ufugaji wa nyuki kwa kuwa ni rahisi lakini unaweza ukasaidia kwa kiwango kikubwa katika kujikwamua kimaisha.
“Mfano mzuri ni mimi mwenyewe, nina mizinga yangu ambayo lengo langu ni kuwa nayo 1,000 ambayo kwa mwaka unaweza ukavuna mara nne na ukauza asali kwa haraka zaidi na bei nzuri,…hivyo angalieni suala hili kwa umakini,” alisema.