Waziri Pinda aanza ziara mkoani Shinyanga

Waziri Mkuu wa Tanzania, Mizengo Pinda

Na Mwandishi Maalumu

WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda leo, Februari 20, 2012, anatarajiwa kuanza ziara ya siku nane mkoani Shinyanga kukagua shughuli za maendeleo katika wilaya zote saba za mkoa huo. Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Waziri Mkuu ataanzia Wilaya ya Maswa, ataenda Bariadi, Meatu, Kishapu, Bukombe, Kahama, Shinyanga Vijijini na kumalizia Shinyanga Mjini.

Katika wilaya zote hizo, Waziri Mkuu atahutubia mikutano ya hadhara na kusalimiana na wananchi kwenye baadhi ya miradi atakayoikagua. Miongoni mwa shughuli ambazo Waziri Mkuu amepangiwa kufanya wakati wa ziara hiyo ni pamoja na kukagua josho la mifugo la Mwamihanza, shamba darasa la pamba, na kukagua mradi wa umeme vijijijini katika kijiji cha Mwandoya wilayani Meatu.

Vilevile, atakagua shamba la mbegu bora ya mtama katika kijiji cha Mwamashele, wilayani Kishapu na shamba la uzalishaji mbegu bora za mihogo katika gereza la Kanegele wilayani Bukombe. Waziri Mkuu pia ataweka jiwe la msingi la mradi wa umwagiliaji maji huko Chela, wilayani Kahama na atakagua na kuweka jiwe la msingi kwenye karakana ya kilimo iliyoko Kahama mjini.

Akiwa Shinyanga, Waziri Mkuu amepangiwa kufungua ghala la mazao la kijiji cha Lyabusalu na kukagua hospitali ya wilaya ya Shinyanga iliyoko Iselamagazi. Kisha atakagua kiwanda cha nyama kilichopo Old Shinyanga na kuzindua Chuo cha VETA Shinyanga.

Februari 27, 2011, Waziri Mkuu atafanya majumuisho ya ziara yake katika mkoa huo kwenye ukumbi wa mikutano wa NSSF na kurejea jijini Dar es Salaam mchana huo huo.