Na Magreth Kinabo-MAELEZO
SERIKALI imeiagiza Menejimenti ya TAZARA kuhakikisha mishahara ya wafanyakazi wake inalipwa haraka, ikiwa ni pamoja na kujenga utaratibu wa kutatua matatizo yanapojitokedha tena kwa muda muafaka.
Kauli hiyo imetolewa jana na Waziri wa Uchukuzi, Omari Nundu alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuhusiana na utendaji wa TAZARA.
“Changamoto zilizopo hivi sasa ni TAZARA kutoweza kulipa mishahara ya wafanyakazi kwa wakati na kutokuwa na mafuta kwa ajili kuendesha treni za abiria. hadi jana kuna baadhi ya wafanyakazi hawakuwa wamelipwa mishahara ya Januari na Februari, mwaka 2010 na wote mishahara ya Februari hawajalipwa .
“Kutokana na hali hiyo wizara imeiagiza menejimenti ya TAZARA ihakikishe kwamba ifikapo Machi 2, 2012 mishahara ya Januari iwe imelipwa na mafuta yawe yamepatikana kwajili ya kuendesha angalau treni tano kwa siku. Mishahara ya Februari nayo ilipwe haraka,” alisema Waziri Nundu.
Aliongeza kuwa tayari menejimenti hiyo imekamilisha taratibu za kuingiza fedha za mishahara ya Januari katika benki, hivyo itawafikia wafanyakazi wa Mbeya Machi 3, mwaka huu na mishahara ya Februari ilipwe katikati ya Machi, mwaka huu. Alifafanua kuwa tayari TAZARA imeshapata lita 600,000 za mafuta, hivyo jana treni nane zimeshanza kufanya kazi kati ya hizo za sita ni za mizigo.
Waziri Nundu alisema mikakati iliyopo sasa ni kuiongezea TAZARA uwezo wa uchukuzi kwa kukarabati injini na mabehewa yaliyopo, kuboresha miundombinu ya reli pamoja na njia za mawasiliano na kuendeleza ushirikiano mzuri wa wateja wakubwa katika kukarabati injini na mabehewa kwa makubaliano maalumu.
Alisema Baraza la Mwaziri la TAZARA limepanga kukutana Mei 23, mwaka huu kujadili masuala ya shirika hilo kwa kina zaidi na kupata ufumbuzi ili kuboresha huduma ziwe za kudumu. Waziri Nundu aliongeza kuwa atakutana na wafanyakazi wa TAZARA Machi 23, mwaka huu na kukagua shughuli za utendaji kazi na njia ya reli kutoka Dares Salaam hadi Tunduma.