Na Mwandishi Wetu
WAZIRI mwenye dhamana ya usimamizi wa sekta za nishati na madini nchini, William Ngeleja ameitaka Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA) kuhakikisha inatoa adhabu kali kwa wafanyabiashara wakaidi wa nishati za mafuta, ikiwezekana kuwafunga ili kudhibiti hujuma ambao wamekuwa wakiifanyia Serikali na wananchi.
Ngeleja ambaye wizara yake pia ni wasimamizi wa nishati hiyo ameitaka EWURA iwachukulie hatua za kisheria ikiwa ni pamoja na kuwasimamisha na kuwafutia leseni wauzaji wa mafuta nchini watakao kiuka kanuni na taratibu walizokubaliana na Serikali.
Ngeleja ametoa kauli hiyo jana Dar es Salaam alipokutana na wamiliki wa vituo vya mafuta na akiwaeleza namna baadhi yao wamekuwa wakikiuka kanuni na taratibu zilizowekwa na Serikali kisheria, jambo ambalo limekuwa likileta usumbufu mkubwa kwa wananchi wanaotegemea nishati hiyo.
Ngeleja alisema licha ya uwepo wa nishati hiyo ya kutosha nchini baadhi yao wamekuwa wakifanya hujuma na kugoma kuiuza nishati hiyo kwa makusudi hali inayoleta usumbufu mkubwa.
“Kuna baadhi ya wafanyabiashara ambao inabidi wachukuliwe hatu kali za kisheria ikiwemo kufungwa kutokana na wao kukiuka agizo la Serikali la kuwataka kuuza mafuta…hali hii imesababisha kuporomoka kwa kiwango cha ukuaji wa uchumi nchini,” alisema Ngeleja.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya EWURA, Haruna Masebu alisema watatekeleza uamuzi wa Serikali ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma hiyo muhimu kwa uhakika, ikiwa ni pamoja na kuwachukulia hatua wale watakaobainika kufanya hujuma kimaslahi yao.
Wafanyabiashara wa mafuta wamekuwa wakiichezea Serikali wanavyotaka, ikiwa ni pamoja na kugoma na kukaidia amri mbalimbali zinazotolewa na mamlaka husika juu ya udhibiti wa nishati hiyo, jambo ambalo limekuwa likiwashangaza wengi.