WAZIRI wa Mambo ya Ndani nchini, Mwigulu Nchemba amefuatilia tukio la kijana Mtanzania anayedaiwa kuteswa na raia wa Kichina wamiliki Mgodi wa Nyamhuna uliopo Katoro-Geita, na kuhakikisha waliohusika na tukio hilo la kumtesa kijana wamekamatwa na Jeshi la Polisi kwa ajili ya hatua zaidi za kisheria. Hii haoa ni kauli yake; “Nimefika Mgodi wa Nyamhuna unaodaiwa kuwa raia wa china ambao ni sehemu ya wamiliki wa mgodi huo wakishirikiana na watanzania walimtesa kinyama na kumjeruhi mmoja wa mtanzania mwenzetu aliyekuwa akifanya kazi katika mgodi huo uliopo Katoro-Geita.
“Imenilazimu kufika gereza la Geita kukutana na kijana huyo ambae yupo hai tofauti na taarifa za awali kuwa alifariki. Baada ya kujiridhisha kuanzia mavazi, majeraha, picha, sura na umbo lake kuwa ndiye kijana aliyeteswa vibaya na picha zake kusambaa mitandaoni na vyombo mbalimbali vya habari, niliamua kwenda naye hadi mgodini lilipofanyika tukio hilo la kinyama, aliwatambua wahusika ambao NI KWELI WALIFANYA TUKIO HILO LA KINYAMA NA LISILOKUBALIKI HAPA NCHINI.”
“Hivyo walioshiriki tukio hilo tumeshawashikilia kupitia jeshi la polisi tayari kwa kufikishwa kwenye vyombo vya sheria. Nalaani tukio hilo vikali sana,serikali hii ipo tayari kushirikiana na kila mmoja rai mwema kutoa taarifa popote pale za matukio au viashiria viovu na vinavyohatarisha usalama wetu. “Usalama wetu,jukumu letu sote,” anasema Waziri Mwigulu Nchemba akizungumzia tukio hilo baada ya kufika eneo la tukio.