Waziri Mkuu wa Uturuki ziarani Somalia

Waziri Mkuu wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan

WAZIRI Mkuu wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan anatarajiwa kuwasili nchini Somalia kuanza rasmi kampeni ya kukabiliana na baa la njaa nchini humo.

Waziri huyo katika ziara yake, ataandamana na Waziri wake wa Mashauri ya Nchi za Kigeni pamoja na wake zao. Viongozi hao wamesema wanakwenda nchini Somalia kuonesha wanawaunga mkono raia wa Somalia katika hali ngumu inayolikabili nchi hiyo.

Hadi sasa raia wa Uturuki wamechangia dola milioni 150 kusaidia Somalia. Bendera za nchi ya Uturuki zimekuwa zikipepea katika uwanja wa ndege na bandari kuu mjini Mogadishu ikiwa ni ishara kuwa mji huo upo tayari kumpokea Waziri Mkuu Erdogan.

Ziara yake huenda ikawa na malengo mawili, moja ni kushuhudia harakati za kusambaza misaada iliochangwa na raia wa nchi yake na pia wana shauku ya kujionea matatizo yanayo wakabili raia wa Somalia.

Ukiachilia mbali misaada ya vyakula na dawa, raia wa Uturuki wamechanga kiasi cha dola 115 milioni kusaidia walioathirika na njaa nchini humo. Serikali ya Uturuki pia imepanga kuongeza ushawishi wake barani Afrika.

Mbali na michango yake kibiashara barani Afrika, Uturuki imeonesha kulithamini bara hilo kwa kiasi kikubwa na kura zake zilisaidia nchi kupata nafasi ilionayo kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Ikiwa Waziri Mkuu, Erdogan atafanikiwa kuchangia kwa kiasi kikubwa mikakati ya kutatua mzozo unaoendelea nchini Somalia- hii itakuwa njia moja ya nchi yake kupewa heshima barani humu na kwenye ngazi za kimataifa.

-BBC