Waziri Mkuu wa Thailand Kutembelea Tanzania Kesho

na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Saidi Meck Sadiki


WAZIRI Mkuu wa Thailand anatarajia kuwasili nchini Tanzania kesho kwa ajili ya ziara ya kikazi. Waziri huyo atawasili nchini Julai 30, 2013 majira ya saa 6:30 mchana. Waziri huyo atalakiwa na mwenyeji wake Rais Jakaya Mrisho Kikwete akifuatana na Viongozi mbalimbali wa Kitaifa na Mkoa.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Saidi Meck Sadiki baada ya kuwasili Waziri Mkuu wa Thailand atakagua gwaride maalum lililoandaliwa kwa ajili yake na pia atapata fursa ya kukagua vikundi mbalimbalivya ngoma ambavyo vitakuwa vikitumbuiza na kutoa burudani kwa Mgeni wetu na msafara wake.

“Mgeni wetu baada ya kukagua vikundi vya ngoma na burudani ataondoka kuelekea Ikulu kupitia barabara ya Nyerere, Railway, Gerezani, Sokoine Drive hadi Ikulu. Akiwa Ikulu atasaini mikataba mbalimbali kati ya Serikali ya Tanzania na Thailand. Usiku atashiriki katika dhifa maalumu iliyoandaliwa na Mwenyeji wake,” ilisema taarifa ya Mkuu wa Mkoa.

“Tunaomba radhi kwamba barabara hizi nilizozitaja zitafungwa kwa muda kupisha misafara ya Viongozi wetu Wakuu watakaoelekea Uwanja wa Ndege wa Kumbukumbu ya Mwalimu J. K. Nyerere kumlaki Mgeni wetu hususan barabara ya Nyerere kuanzia saa 6.00 mchana hadi saa 7.30 mchana.” Ilisema taarifa hiyo.

Akifafanua zaidi juu ya ziara ya waziri mkuu huyo, Mkuu wa Mkoa alisema Julai 31, 2013 Waziri Mkuu wa Thailand atatembelea Mbuga za Wanyama za Serengeti, na Agosti 01, 2013 atarejea Dar es Salaam na kuagwa rasmi katika Uwanja wa Mwalimu Julius Nyerere na kuendelea na ziara yake huko Uganda.

Kama ilivyo ada tunaombwa kumlaki mgeni wetu kwa shangwe na bashasha katika maeneo yote atakayopita.