Waziri Mkuu wa India kuja Tanzania

TAARIFA KWA MHARIRI

Waziri Mkuu wa India, Mheshimiwa Manmohan Singh amekubali mwaliko wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete kutembelea Tanzania wiki ijayo.

Mheshimiwa Singh amekubali mwaliko huo katika barua yake aliyomwandikia Rais Kikwete na iliyokabidhiwa kwake na Balozi wa India katika Tanzania, Mheshimiwa K.V. Bhagirah wakati Balozi huyo alipokutana na kufanya mazungumzo na Rais Kikwete leo, Alhamisi, Mei 19, 2011, Ikulu, Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa mwaliko wa Rais Kikwete uliokubaliwa na Mheshimiwa Manmohan Singh, Waziri Mkuu huyo wa India atakuwa nchini kwa siku mbili za ziara rasmi kuanzia Mei 26.
Katika barua yake kwa Rais Kikwete, Mheshimiwa Singh amesema: ÒNakushukuru kwa barua ya kunilialika kuitembelea nchi yako nzuri. Itakuwa ni heshima kwangu kuitembelea Tanzania na naukubali mwaliko huo kwa furaha kubwa.Ó

Ameongeza Waziri Mkuu huyo: ÒNina ari kubwa kukutana nawe na marafiki wengine wa Tanzania wakati wa ziara hiyo na kujadili njia ya kuuinua uhusiano kati ya nchi zetu kwenye ngazi mpya kwa manufaa ya wananchi wa nchi zetu mbili.Ó

Kabla ya kuja Tanzania, Mheshimiwa Singh atahudhuria Mkutano wa Pili kati ya India na Afrika utakaofanyika mjini Addis Ababa, Ethiopia, ambako Bara la Afrika litawakilishwa na wakuu wa jumuia za uchumi za Afrika.

Mkutano wa kwanza kati ya India na Afrika uliofanyika mwaka 2008 ulikuwa chini ya uenyekiti wenza wa Rais Kikwete na Waziri Mkuu Singh na ulifungua ukusara mpya katika mahusiano kati ya pande hizo mbili. Wakati huo, Rais Kikwete alikuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU).

Tanzania na India zimekuwa na uhusiano wa kihistoria ambako viongozi wa juu wa nchi hizo zimefanya ziara za kubadilishana na biashara kati ya nchi hizo mbili imefikia thamani ya dola za Marekani bilioni 1.1. Uwekezaji wa makampuni ya India katika uchumi wa Tanzania unakadiriwa kufikia kiasi cha dola za Marekani bilioni 1.3.

Imetolewa na:

Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.

19 Mei, 2011