RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete Septemba 5, 2012, amekutana na kufanya mazungumzo na Naibu Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Watu wa China, Hui Liangya kuhusu masuala mbali mbali yanayohusu uhusiano kati ya nchi hizo mbili.
Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika Ikulu, Dar es Salaam mara tu baada ya Liangya kuwasili nchini kwa ziara ya siku tatu katika Tanzania kama sehemu ya ziara ya nchi za Afrika, viongozi wote wawili wameeleza kuridhishwa kwao na hali na ustawi wa uhusiano kati ya nchi hizo mbili.
Rais Kikwete ametumia nafasi ya ziara hiyo ya Liangya kuishukuru China kwa michango yake katika jitihada za maendeleo za Tanzania.
Amesema Rais Kikwete: ”Jamhuri ya Watu wa China imetusaidia mengi katika jitihada zetu za maendeleo kuanzia kwenye ujenzi wa Reli ya TAZARA, ujenzi wa Uwanja wa Taifa, ujenzi wa Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere, ujenzi wa bomba la gesi kutoka Mtwara hadi Dar Es Salaam, ujenzi wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano, na ahadi ya kusaidia kuanzisha Benki ya Kilimo Tanzania. Kwa hakika Jamhuri ya Watu wa China imetusaidia mengi na tunaishukuru sana.”
Rais Kikwete pia ameitaka China kuendelea kuisaidia Tanzania hasa katika maeneo ya jinsi ya kuongeza kasi ya uchumi. “Tunataka kwa kweli kujifunza kutoka mifano ya mafanikio ya marafiki zetu wa karibu kama China. Hivyo, bado tunaendelea kusisitiza ushirikiano wa China katika kuanzisha na kuendesha maeneo maalum ya uzalishaji –Special Economic Zones “
Naye Liangya amemwambia Rais Kikwete kuwa China itaendelea kuimarisha uhusiano wake na Tanzania ambao umekuwa unashamiri tokea ulipoanzishwa na Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere na Mwenyekiti Mao Tse Dung.
Liangya amesema kuwa undani wa miradi yote ambayo China inasaidia katika Tanzania ungejadiliwa kwenye mkutano kati yake na Waziri Mkuu Mizengo Pinda katika mazungumzo rasmi yaliyofanyika baada mchana wa leo.
Kiongozi huyo wa China pia ameisifu Serikali ya Kikwete kwa uamuzi wake wa kuanzisha Mpango wa Maendeleo wa Miaka mitano na kuongeza kuwa mpango huo umeandaliwa kwa umakini mkubwa. “Nawapongezeni kwa uamuzi wenu wa busara wa kuanzisha tena Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano. Ukitekelezwa vizuri unaweza kusukuma kwa kasi zaidi maendeleo ya nchi yetu.”