Waziri Mkuu Uingereza aitisha Bunge la dharura

Waziri Mkuu, David Cameron

BUNGE la Uingereza linatarajiwa kufanya kikao cha dharura baadaye leo kujadili juu ya ghasia ambazo zimeikumba miji kadhaa nchini humo. Taarifa zinaeleza Waziri Mkuu, David Cameron atawasilisha taarifa ya Serikali pamoja na harakati za polisi katika kuthibiti ghasia na uporaji huo.
Hii ni mara ya tano wabunge Uingereza wamelazimika kukatiza likizo zao katika miongo mitano. Waziri Mkuu Cameron hii itakuwa mara yake ya pili kuitisha kikao cha dharura akiwa madarakani, awali ikiwa kujadili sakata ya udukuzi wa simu hivi karibuni.
Tukio la sasa linaonekana kuwa na uzito mkubwa kutokana na kwamba ni wajibu wa Serikali kuhakikishia wananchi wake wapo salama pamoja na utekelezwaji wa sheria nyingine.
Changamoto kubwa inayomkabili David Cameron ni kuishawishi bunge kwamba serikali yake imeweza kuthibiti hali kwa sasa. Cameron ametaja machafuko ya sasa kama vitendo vya jinai na kutowajibika wala siyo kero za tofauti za kijamii na gharama za maisha.
Msimamo huu unaonekana samba mba na maoani ya raia wengi, japo wamelaumu serikali hususan idara ya polisi kwa kutochukua hatua madhubuti kukabiliana na makundi yaliyozua rabsha na kupora mali.
Polisi wamekuwa wakishika doria katika miji ya Uingereza kuzuia tukio jingine.Kwa sasa hali ya utulizu umerejea kutokana na idadi ya polisi wanaoshika doria pamoja na mvua kubwa ambayo imenyesha maeneo yaliyoathirika.
Tayari Waziri Mkuu amesema njiya mbadala za kuzima ghasia zitatumiwa ikiwemo maji ya kuwasha. Cameron amezuru mji wa Birmingham kufariji familia za watu watatu waliogongwa na gari wakati wakijaribu kulinda mali zao.
-BBC