Waziri Mkuu Pinda kufunga Maonesho ya Miaka 50 ya Uhuru Dar

Waziri Mkuu wa Tanzania, Mizengo Pinda

Na Mwandishi Wetu

WAZIRI Mkuu wa Tanzania, Mizengo Pinda Desemba 12, 2011 anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika shughuli maalum ya kufunga Wiki ya Maonesho ya Maadhimisho ya Miaka 50 ya Uhuru itakayofanyika kwenye Viwanja vya Mwalimu J. K. Nyerere, barabara ya Kilwa jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo kwa vyombo vya habari Dar es Salaa na Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Peniel Lyimo imesema Waziri Mkuu anatarajiwa kuwasili viwanja hivyo saa 3.30 asubuhi hivyo kuwaomba washiriki wote kuwahi mabandani mwao mapema asubuhi.

Mara baada ya kuwasili, Waziri Mkuu Pinda atatembelea mabanda ya washiriki mbalimbali ili kujionea shughuli zilizozokuwa zikifanyika na baadaye atawahutubia washiriki wa maonesho hayo kabla ya kuyafunga rasmi.
Maonesho hayo yanayoshirikisha wizara, mikoa na taasisi mbalimbali, sekta binafsi na wafanyabiashara mbalimbali wa kimataifa na ndani ya nchi yalianza Desemba Mosi, 2011 katika viwanja hivyo na kufunguliwa rasmi Desemba 2, 2011 na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein. Maonesho hayo yalikuwa ni ya bure kwa wananchi wote.

Viongozi wa kitaifa waliopo madarakani na wastaafu wametembelea maonesho hayo kwa nyakati mbalimbali.
Maadhimisho ya Miaka 50 ya Uhuru yalizinduliwa rasmi Juni Mosi, 2011 mjini Songea na Makamu wa Rais, Dk. Mohamed Gharib Bilal ambapo mambo mbalimbali yamefanyika hadi sasa. Miongoni mwa shughuli za maadhimisho hayo ni maonesho yaliyoshirikisha Wizara, Mikoa na Sekta Binafsi ambayo yalikamilika Novemba 30, 2011.

Vilevile kulikuwa na taarifa za Miaka 50 ya Uhuru zilizoandaliwa na Wizara na Mikoa ambazo pia zimetumika pia katika kuandaa Taarifa Jumuishi ya Kitaifa iliyochapishwa kwa Kiswahili na Kiingereza. Taarifa hizo zimewekwa kwenye Tovuti ya Taifa, Tovuti ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Tovuti maalum iliyoanzishwa kwa ajili ya maadhimisho hayo.

Shughuli nyingine maalum iliyofanyika wakati wa maadhimisho hayo ni Mbio za Mwenge wa Uhuru ambazo zilitumika kuelezea mafanikio ya Serikali katika kipindi cha miaka 50. Mwenge huo uliwashwa rasmi na Makamu wa Rais, Dkt. Bilal katika kijiji cha Butiama tarehe 14 Oktoba, 2011 na mbio hizo zilifikia kilele Desemba Mosi, 2011 jijini Dar es Salaam ambapo Rais Jakaya Kikwete alipokea mwenge huo katika Uwanja wa Uhuru na kuwakabidhi wanajeshi waliopewa jukumu la kuupandisha katika Mlima Kilimanjaro.