WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda kesho Desemba 11, 2012 anatarajiwa kuanza ziara ya siku 13 kwenye jimbo la Katavi wilayani Mlele, mkoani Katavi ambako atatembelea kata zote za wilaya hiyo,
atafanya mikutano ya hadhara na kukagua baadhi ya miradi ya maendeleo.
Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Waziri Mkuu ataanzia kata ya Inyonga, Ilunde, Ilela, Nsenkwa, Utende na Uruwira. Baada ya hapo atakwenda kata za Ugalla, Litakumba, Nsimbo, Kapalala, Mtapenda, Kasokola, Magamba, Itenka, Machimboni, Sitalike, Kibaoni, Kasansa na Mamba.
Katika duru ya mwisho, Waziri Mkuu atatembelea kata za Majimoto, Mwamapuli, Usevya, Mbede, Ikuba na kurejea tena Kibaoni ambako atakuwa na mapumziko ya Krismasi.
Baadhi ya shughuli kubwa ambazo Waziri Mkuu amepangiwa kufanya wakati wa ziara hiyo ni pamoja na kuzungumza na wananchi kwenye mikutano ya hadhara katika kila kata, kufungua mabweni na kukagua ujenzi wa nyumba za walimu katika sekondari ya Ilela, kuweka jiwe la msingi la zahanati ya Nsenkwa, kukagua kituo cha afya na kuzindua mradi wa madawati kwa
shule za tarafa ya Inyonga.
Waziri Mkuu pia atakagua miradi ya kilimo Mwamapuli na pia anatarajiwa kuzindua mradi wa umeme jua kwenye shule ya sekondari ya Usevya. Mkoa mpya wa Katavi ambao ulizinduliwa rasmi Novemba 25, mwaka huu na Makamu wa Rais, Dk. Gharib Mohammed Bilal, una wilaya mbili za Mpanda na Mlele. Pia una majimbo matatu ya uchaguzi ambayo ni Katavi, Mpanda Mjini na Mpanda Vijijini.