Waziri Mkuu Pinda Azinduwa Chama cha Wafuga Nyuki

Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akizungumza.

Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akizungumza.


WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda amezindua Chama cha Kuendeleza Ufugaji Nyuki Tanzania (Tanzania Beekeeping Development Organization – TABEDO) na kukitaka kishirikiane na makampuni binafsi ili kuendeleza sekta hiyo kwa haraka. Ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na washiriki zaidi ya 100 kutoka mikoa yote ya Tanzania Bara na Visiwani ambao walishiriki uzinduzi wa chama hicho uliofanyika mjini Dodoma.

“Ushiriki wa sekta binafsi katika uzalishaji na uwekezaji viwanda vinavyojikita katika ufugaji nyuki bado ni mdogo sana hapa nchini. Naamini TABEDO ikishirikiana na sekta binafsi itakuwa chachu katika kukuza sekta hii ya ufugaji nyuki hapa Tanzania. Viongozi wa Chama hiki hawana budi kuhakikisha wanahamasisha makampuni ya watu binafsi ya ndani na nje ya nchi, vyama vya ushirika na taasisi zisizo za kiserikali wajiunge na TABEDO ili muwe na wigo mpana wa kuendeleza sekta hii,” alisema.

TABEDO kinaundwa na wafugaji nyuki, wachakataji na wafanyabiashara wa mazao ya nyuki, watengenezaji na wasambazaji wa vifaa vya ufugaji nyuki. Waziri Mkuu amesema taarifa za wachambuzi wa biashara ya mazao ya nyuki kimataifa zinaonyesha kuwa soko la asali ulimwenguni linategemea kuongezeka hadi kufikia tani millioni 1.9 zenye thamani ya Dola za Kimarekani billioni 12 kwa mwaka huu. Alisema soko la Jumuiya ya Nchi za Ulaya linaongezeka kwa asilimia 2.5 kila mwaka. Na kwamba jambo hilo limetokana na viwango vya uelewa wa faida za matumizi ya mazao ya nyuki na kutambua umuhimu wake katika kuboresha afya kwa walaji au watumiaji.

“Hapa nchini, wastani wa bei ya asali katika soko la ndani ni Sh. 6,000 – 8,000 kwa kilo moja, (Dola za Kimarekani 3.60) na ile ya soko la nje ni Dola za Kimarekani 3.5 sawa na shilingi 7,525 kwa kilo. Wastani wa bei ya nta ni sh. 8,000 kwa kilo (Dola za Kimarekani 5) na kwenye soko la nje ni wastani wa Dola za Kimarekani 8.9 kwa kilo sawa na sh. 19,135,” alisema.

Alisema takwimu hizo zinaonesha kuwa mazao ya nyuki yana bei nzuri ndani na nje ya nchi hivyo kinachotakiwa ni kuongeza uzalishaji na ubora wa mazao ya nyuki kwa kuzitumia taasisi za serikali na zisizo za kiserikali kama Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) na Global Standard 1 (GS1). “Bidhaa ikipata alama za taasisi zote hizi itauzika kwa urahisi sana kwenye maduka makubwa (supermarkets) kwa bei nzuri zaidi. Natoa rai chama hiki kiwashawishi wanachama wake kupata vyeti kutoka taasisi hizi ili muweze kuongeza mauzo ya mazao ya nyuki na hatimaye kujiongezea kipato,” alisema.

Alisema asali ya Tanzania ni miongoni mwa asali bora na nzuri sana ulimwenguni kwani inatokana na misitu ya asili ambayo ipo huru na kemikali zinazotokana na shughuli za kilimo. Tanzania huzalisha aina mbali mbali za asali kulingana na utajiri wa uoto na aina za mimea iliyopo nchini. Ni dhahiri kuwa asali inayotokana na karafuu kule Pemba, vichaka vya Itigi (Itigi thickets), Migunga (Acacia) kule Katavi, Ludewa na Igunga inaweza kuongeza thamani ya asali na vilevile kuwa na viini lishe na tiba tofauti za asali nyingine ya kawaida.

Alisema taarifa hizi bado haijaelezwa au hazifahamiki kwa wengi ndani na nje ya nchi, hivyo, kuna umuhimu wa kufanya utafiti wa kina wa asali hizi ili kubaini viini lishe na tiba sahihi kwenye asali hizi. Alisema hatua hiyo, itasaidia kuongeza thamani katika soko la dunia na kutambulika kwa njia ya branding.

Ameiagiza Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kushikirikiana na taasisi za utafiti za ndani na nje ifanye tafiti za kutambua viambato vilivyopo kwenye asali kutoka kwenye maeneo mbalimbali ili kurahisisha kazi ya branding kwa zao asali.

Waziri Mkuu alisema Serikali imeandaa mikakati ya kukuza tafiti katika ufugaji wa nyuki ili kuipa hadhi asali ya Tanzania. “Ujenzi wa maabara ya asali unaendelea katika Kituo cha Utafiti wa Nyuki Njiro, Arusha. Maabara hii ikikamilika itawezesha wafugaji nyuki na wadau wengine kuhakiki ubora wa mazao na kupata hati ya kuthibitisha ubora wa mazao kwa bei nafuu,” aliongeza.

Alisisitiza kwamba taasisi hiyo itakuwa kiungo cha kupashana habari za ufugaji nyuki ambazo katika ulimwengu wa sasa kibiashara ndizo zinazoongeza thamani ya bidhaa katika soko. “Pia taasisi hii itatoa majibu ya changamoto zinakabili sekta ndogo ya ufugaji nyuki kupitia tafiti zitakazokuwa zikiendeshwa,” alisema.