Waziri Mkuu Pinda Awaagiza Wakuu wa Mikoa ‘Kushiriki’ Maonesho ya Asali

Waziri Mkuu wa Tanzania, Mizengo Pinda

Na Mwandishi Maalumu

WAZIRI
Mkuu Mizengo Pinda amewataka Wakuu wa Mikoa kuhakikisha wanatuma wawakilishi kwenye Maonesho ya Asali Kitaifa yanayotarajiwa kufanyika jijini Dar es Salaam kuanzia Oktoba 3 – 7, mwaka huu.

“Mikoa yote itume wawakilishi ili waje kushiriki maonesho haya. Tumeweka vigezo vya kushindanisha mikoa mbalimbali na wafugaji nyuki wa kawaida. Natoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi ili waone fursa zilizopo kwenye sekta hii ili waweze kushiriki kukuza uchumi wao binafsi na wa Taifa pia,” alisema.

Waziri Mkuu ametoa wito huo Septemba 20, 2012 na kusisitiza kuwa Halmashauri zote nchini zilikwishapelekewa barua ya kuwataka washiriki maonesho hayo lakini hadi sasa ni Halmashauri 50 tu ambazo zimethibitisha kushiriki. Tanzania kuna jumla ya Halmashauri 133.

Halmashauri ambazo zimethibitisha kushiriki ni Manispaa ya Iringa, Manispaa ya Tabora, Manispaa ya Kigoma-Ujiji, Mji-Njombe, Mji-Mpanda, Halmashauri za Wilaya za Babati, Simanjiro, Kondoa, Mpwapwa, Kongwa, Iringa, Ludewa, Makete, Mufindi, Njombe, Kibondo, Kigoma, Mwanga na Same.

Nyingine ni Halmashauri za Wilaya za Kilwa, Lindi, Ruangwa, Liwale, Nachingwea, Serengeti, Chunya, Kilombero, Kilosa, Kwimba, Bagamoyo, Kibaha, Kisarawe, Mpanda, Sumbawanga, Muheza, Korogwe na Handeni. Nyingine ni Halmashauri za Wilaya za Urambo, Tabora, Sikonge, Nzega, Kahama, Bukombe, Bariadi, Singida, Iramba, Manyoni, Kilolo, Mkinga na Missenyi.

Akisisitiza umuhimu wa Maonyesho hayo ya Asali Kitaifa, Waziri Mkuu alisema: “Maonyesho ni kama shamba-darasa, ukipita mwanzo hadi mwisho unajifunza kitu cha ziada… ukitoka hapo ni lazima utapata hamasa fulani. Kama kuna jambo ulishafanya kuhusiana na kile ulichoona, basi ukipita katika maonyesho utajifunza kitu kipya na kwenda kuboresha kile cha kwako,” alisema Waziri Mkuu.

Alisema watu watakaoshiriki maonyesho hayo watajifunza aina mbalimbali za mizinga ya nyuki, aina za asali, faida za asalai kama chakula na dawa, wataona asali zenye ladha (aroma) tofauti, pia wataona mazao mbalimbali yatokanayo na ufugaji nyuki kama vile nta, propolis na royal jelly.

Alisema kila mwaka watu mbalimbali walikuwa wakishiriki maonyesho ya nanenane lakini ni wachache sana waliokuwa wakijitokeza kushiriki ama kuhudhuria maonesha hayo. “Sasa tumeamua tunataka tuone wadau wote, waoka mikate na keki ambao wanatumi asali, watengeneza vipodozi, wajasiriamali, halmashauri na wadau kutoka nje ya nchi,” alisema.

Maonesho hayo ambayo kaulimbiu yake ni “Asali kwa Afya na Ustawi” yamepangwa kufanyika katika Uwanja wa Maonesho wa Mwl. J. K. Nyerere, barabara ya Kilwa kuanzia Oktoba 3-7, 2012 ambapo yatatanguliwa na kongamano kubwa la wadau wa sekta ya nyuki litakalofanyika tarehe 3 Oktoba, mwaka huu.

Desemba 12, 2011 wakati akifunga maadhimisho ya miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania, Waziri Mkuu Pinda aliagiza yaandaliwe maonesho makubwa ya asali ambayo yatatambulisha sekta hii na fursa zake ili kufungua mianya ya uwekezaji na uendelezaji wa biashara katika sekta ya nyuki.

Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE) inasimamia jukumu la kuandaa maonyesho hayo kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu, Ofisi ya Makamu wa Rais – Mazingira, Wizara ya Maliasili na Utalii, Wizara ya Viwanda na Biashara, Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika na asasi za Serikali na sekta binafsi.