WAZIRI Mkuu wa Tanzania, Mizengo Pinda ameunda Tume maalum itakayofanya uchunguzi wa matokeo ya mtihani wa kidato cha nne ya 2012, ambayo yamezua mgogoro mkubwa baada ya kutoka hivi karibuni na idadi kubwa ya wanafunzi waliofanya mtihani huo kufeli.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari na Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Bw. Peniel Lyimo tume iliyoundwa inatarajiwa kuanza kazi wakati wowote kuanzia wiki ijayo.
Katibu Mkuu huyo wa Ofisi ya Waziri Mkuu, alisema Tume hiyo inajumuisha wadau kutoka Chama cha Wamiliki wa Shule na Vyuo Binafsi (Tanzania Association of Managers and Owners of Non-Government Schools/Colleges (TAMONGSCO), Taasisi za Dini zinazotoa huduma ya elimu, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Asasi zisizo za Kiserikali (NGOs) zinazoshughulikia masuala ya elimu.
Lyimo alisema wadau wengine katika tume hiyo watatoka Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Kamati ya Bunge ya Huduma za Jamii na Umoja wa Wakuu wa Shule za Sekondari Tanzania (TAHOSSA).
“…Serikali inawaomba wadau wa elimu, wazazi, walezi na wananchi wote kwa ujumla watoe ushirikiano kwa Tume ili iweze kufanya kazi yake kwa ufanisi.” Alisema katika taarifa hiyo.
Februari 18, 2013, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa alitangaza matokeo ya kidato cha nne ya mwaka 2012 ambapo asilimia 60 ya wanafunzi waliofanya mtihani huo walifeli jambo ambalo limezua mvutano mkubwa.