WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda ameongoza harambee ya papo kwa papo na kufanikiwa kukusanya sh. milioni 31.5 zikiwa ni ahadi na fedha taslimu kwa ajili ya ukarabati wa Kanisa Katoliki la Mashahidi wa Uganda la Magomeni, jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na waumini wa Kanisa hilo Machi 17, 2013 kabla ya kuendesha harambee hiyo, Waziri Mkuu aliusifu uongozi wa Kanisa Katoliki la Magomeni kwa kuamua kufanya upanuzi wa kanisa hilo ili liweze kuhudumia waumini wengi zaidi.
“Nia yao ni nzuri sana na wameona mbali mapema. Magomeni hii ya leo si ya wakati ule, na wala haitakuwa hivi katika miaka mingine 50 ijayo. Zamani usingeweza kuona hata ghorofa moja hapa Magomeni lakini sasa hivi maghorofa hayahesabiki,” alisema.
Aliwasisitiza waumini hao kujitoa kwa ajili ya kazi ya Bwana kwa sababu hakuna sadaka ambayo ni ndogo. “Hakuna sadaka iliyo ndogo mbele ya Mungu, kikubwa ni dhamira tu. Kanisa ni letu na litajengwa na sisi waumini ili mradi kila mmoja wetu aseme Kansa hili nitalijenga,” alisisitiza.
Mapema akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na waumini hao, Baba Paroko wa kanisa hilo, Padri Sixfrious Rwechungura alisema wameanza kazi ya ukarabati tangu Agosti 15, 2011 na kwamba hadi sasa wamekwishakusanya sh. milioni 350 iliyotokana na nguvu za waumini wenyewe bila msaada wa kutoka nje.
Alisema wanahitaji kiasi cha sh. milioni 300 ili kukamilisha kazi hiyo ambayo inapaswa kukamilika katika miaka miwili ijayo ili iendane na maadhimisho ya miaka 50 ya kanisa hilo.
Katika harambee hiyo, Waziri Mkuu na mkewe Mama Tunu Pinda waliahidi kuchangia sh. Milioni 10 na kutoa sh. Milioni mbili za kianzio. Pia aliendesha mnada wa mbuzi aliyenunuliwa kwa sh. 600,000/- na mkoba ulionunuliwa kwa sh. 150,000/-.