Waziri Mkuu Pinda Ahaidi Neema Mtwara Kumaliza Mzozo

Waziri Mkuu na jopo la Mawaziri kikaoni mkoani Mtwara kutafuta muafaka. (Picha na Mtwara Kumekucha blog)

*Asema Mtwara Corridor itapewa kipaumbele

WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda amesema Serikali italipa uzito wa kipekee suala la uendelezaji wa Ukanda wa Kiuchumi wa Mtwara (Mtwara Corridor) kama ilivyo kwa Ukanda wa Kilimo wa Nyanda za Juu Kusini Tanzania (SAGCOT). Amesema Serikali itachukua hatua hiyo ili kuiendeleza kiuchumi mikoa ya kusini ambayo ni Lindi, Mtwara na Ruvuma.

Ametoa kauli hiyo Januari 30, 2013 mjini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari ili kutoa ufafanuzi juu ya suala alilokwenda kufuatilia mkoani Mtwara kufuatia vurugu zilizozuka hivi karibuni kuhusiana na suala la uchimbaji gesi mkoani humo.

Mbali na hilo, Waziri Mkuu amesema Serikali itahakikisha Wizara ambazo zinawajibika kutoa maelezo kuhusu uwekezaji na uendelezwaji wa miradi mkoani Mtwara zinaweka ratiba maalum ya kwenda huko na kutoa maelezo ya kina kwa wananchi. Alitumi fursa hiyo kuwasihi wakazi wa mkoa huo kuhakikisha kuwa amani na utulivu vinaimarishwa kama kweli wanataka mkoa huo uendelezwe.

“Ninawasihi wakazi wa Mtwara waimarishe amani na utulivu sababu fursa walizonazo ni kubwa sana. Ni vizuri viongozi na wananchi wa mkoa huo wakajipanga vizuri ili waangalie namna watakavyonufaika na uwekezaji huo,” alisema.

Akifafanua kuhusu mgogoro uliosababisha vurugu hizo, Waziri alisema katika muda wa siku mbili alizokuwa Mtwara aliweza kukutana na vikundi tisa vilivyojumuisha viongozi wa dini, viongozi wa vyama vya siasa, madiwani, wafanyabiashara na vyombo vya dola.

Alisema baada ya kusikiliza pande zote, Waziri Mkuu aliwaita mawaziri wa Elimu, Uchukuzi, Ardhi na Maendeleo ya Makazi, Viwanda na Biashara na Kaimu Mkurugenzi wa TIC ili watoe ufafanuzi kwenye kikao cha majumuisho ambacho kilifanyika jana (Jumanne, Januari 29, 2013) mjini Mtwara.

“Ni bahati mbaya hali ilikuwa hivyo. Ni jambo ambalo lisingetakiwa kufika hapo. Ni bahati mbaya kwamba elimu kuhusu uwekezaji mkoani Mtwara haikuwa imefika kwa wananchi walio wengi, ni wananchi wachache waliofikiwa wakati wa kutoa taarifa. Wabunge walijua jambo hili na walikuwa na wajibu wa kuwaelimisha wananchi…,” alisema.

Waziri Mkuu alisema hoja kuu iliyotolewa na wakazi hao ni kwamba walikuwa hawapingi gesi kwenda Dar es Salaam isipokuwa walikuwa wakitaka kijengwe kiwanda cha kusafisha gesi pale Mtwara ili mabaki yanayotokana na usafishaji huo yatumike palepale mkoani kutengenezea bidhaa nyingine kama vile mbolea na vifaa vya plastiki.

Akielezea kuhusu hasara zilizosababishwa na vurugu hizo, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi alisema nyumba, ofisi na magari vilichomwa moto katika sakata hilo lililohusisha wilaya za Mtwara na Masasi Januari 25 na 26 mwaka huu.

Alibainisha kwamba kwa wilaya ya Masasi pekee gharama za kurekebisha uharibifu huo zinafikia sh. bilioni 1.5/-. Hata hivyo, alisema gharama halisi za uharibifu uliotokea kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara pamoja na Manispaa ya Mtwara hazikuweza kupatikana kwa haraka.