WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amewaasa raia wanaokimbia nchi zao na kupata hifadhi Tanzania kutobeba silaha wanapoingia nchini kuja kuishi kwenye kambi za wakimbizi. Ametoa onyo hilo Desemba 29, 2015 na wakati akizungumza na mamia ya wakimbizi wanaoishi kwenye kambi za Nyarugusu na Nduta zilizoko wilayani Kasulu na Kibondo, mkoani Kigoma waliofika kumsikiliza kwenye mikutano ya hadhara iliyofanyika kwenye kambi hizo.
“Ninawasihi mjitambue kuwa mmehama kutoka DRC na Burundi, na mnapoingia hapa inabidi mbadilike muwe na tabia za hapa. Hatuhitaji mje na silaha au vifaa hatarishi kwa sababu tunataka mkae kwa usalama,” alisema.
Alisema suala la usalama ni muhimu miongoni mwao, ni muhimu zaidi kwa majirani zao lakini pia ni muhimu sana kwa watoa huduma wanaowahangaikia. “Tunataka kila mmoja awe mlinzi wa mwenzake ili siku mkiondoka mrudi nyumbani mkiwa salama,” alisema.
“Ninyi mko hapa mnatunzwa kwa hiyo hamruhusiwi kutoka kambini na kutembea hovyo huko nje. Hii ni kwa usalama wenu. Hatumruhusu kuingia na bunduki au mabomu na yeyote atakayemuona mwenzie ana silaha au ameificha mahali aje atuambie ili tumchukulie hatua na ninyi wengine mbakie salama,” alisisitiza.
Kuhusu maambukizi ya Virusi vya UKIMWI (VVU), Waziri Mkuu aliwataka wakimbizi hao wajiepushe na ngono zembe kwa sababu kiwango cha maambukizi kimeongezeka kwa asilimia moja ikilinganishwa na mwaka jana.
“Nimetembelea hospitali yenu hapa kambini na kuelezwa kuwa maambukizi ya VVU hapa yapo na mwaka huu yamefikia asilimia mbili ya watu waliopimwa ikilinganishwa na mwaka ambapo ilikuwa ni asilimia moja tu,”
“Kutokana na uwingi wenu, naomba niwasihi sana mjizuie kufanya ngono zembe na kama mtu atashindwa kabisa kujizuia ni vema atumie kinga. La sivyo mtaleta maambukizi ya juu sana na wote mtakwisha,” alisema.
“Suala lenyewe siyo jambo la dharura, kawaida huwa kuna maandalizi baina ya wahusika, watu wanakubaliana juu ya muda na mahali pa kukutanandiyo maana nasema siyo jambo la dharura. Ndugu zangu tujihadhari sana kwa sababu kasi ya maambukizi mahali hapa iko juu sana,” alisisitiza.
Mapema, Mkuu wa kambi ya Nyarugusu, Bw. Sospeter Boyo alimweleza Waziri Mkuu kwamba kambi hiyo ilifunguliwa Novemba 1996 kwa lengo la kuwahifadhi wakimbizi kutoka Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo waliokuwa wakikimbia vita ya wenyewe kwa wenyewe. Alisema kambi hiyo yenye ukubwa wa kilometa za mraba 28, ina uwezo wa kuhifadhi wakimbizi 50,000 lakini kwa sasa inao wakimbizi 151,032 ambao ni mara tatu zaidi ya uwezo halisi wa kambi hiyo.
“Tangu Aprili mwaka huu, idadi ya wakimbizi imeongezeka hadi kufikia 151,032 miongoni mwao ni wakongo 61,313, warundi 89,619, Wanyarwanda 75, Waganda 12, Wasudan kusini wane, Wakenya wane, Msomali mmoja, Mzimbabwe mmoja na raia wa Ivory Coast mmoja,” alisema Bw. Boyo.
Alisema wanakabiliwa na changamoto za uhaba wa maji safi, ufinyu wa huduma za afya na elimu na uharibifu wa mazingira. Waziri Mkuu bado anatembelea pia kambi ya JKT ya Mtabila wilayani Kasulu na kesho asubuhi anatarajiwa kufanya majumuisho ya ziara yake.