Ametoa kauli hiyo wakati akizungumza kwa nyakati tofauti kwenye mikutano ya hadhara iliyofanyika Desemba 21, 2015 kwenye vijiji vya Nangurugai, Machang’anja na Narungombe katika kata za Mbwemkuru na Narungombe wilayani Ruangwa, mkoani Lindi.
Waziri Mkuu alikuwa akijibu hoja za diwani wa Narungombe, Bw. Rashid Nakumbya aliyetoa ombi la kuongezewa chakula cha msaada kwa sababu wana hali mbaya. Alisema msimu uliopita haukuwa mzuri kiuzalishaji kutokana na hali mbaya ya hewa. Pia aliomba wasaidiwe kuboreshewa huduma za maji safi na salama.
“Natambua kuwa kuna tani 2,000 za chakula zimeletwa katika mkoa wetu lakini hizo hazitoshi kwa sababu mahitaji yetu ni zaidi ya tani 5,000. Chakula hiki hakitoshi kwa sasa lakini kitasaidia kupunguza makali ya njaa,” aliwaeleza wakazi hao.
“Tumepiga marufuku kutumia chakula cha msaada kupikia pombe. Mwananchi atakayekutwa akitumia chakula hicho, atachukuliwa hatua za kinidhamu,” alisisitiza.
Alitumia fursa hiyo kuwahakikishia kauli ya Rais Dk. John Pombe Magufuli kwamba hakuna mwananchi atakayekufa kwa njaa. “Mheshimiwa Rais ameahidi kuwa hakuna Mtanzania atakayekufa kwa njaa. Tuna mahindi ya kutosha kwenye maghala ya Songea, Dodoma na Makambako lakini changamoto ni namna ya kuyasafirisha kutoka huko hadi kuyafikisha huku. Tunaendelea pia kupeleka misaada kwenye mikoa mingine,” alisema Waziri Mkuu.
Akijibu hoja nyingine zilizotolewa, Waziri Mkuu ambaye pia ni mbunge wa jimbo hilo alisema anatambua changamoto walizonazo za ukosefu wa maji safi, ubovu wa barabara, zahanati na nyumba za waganga na kwamba ameanza kuzishughulikia.
“Hivi sasa nimeanza kushughulikia suala la uwekaji wa nishati ya umeme wa jua kwenye shule za msingi na zahanati. Mtaalam ameshafika hapa wilayani kwetu na ameanza hiyo kazi, na hivi karibuni mtamuona akifika maeneo ya huku,” alisema.
Kuhusu maji safi na salama, Waziri Mkuu aliwaeleza wakazi hao kwamba tatizo la maji analijua na kwamba changamoto kubwa waliyonayo ni upatikanaji wa chanzo cha maji baridi kwani kiasi kikubwa eneo hilo lina vyanzo vya maji yenye chumvi. “Wataalamu wanakuja kutafuta chanzo cha maji baridi kwa sababu asilimia kubwa ya eneo hili maji yake yana chumvi,” alisema.
Aliwataka wakazi hao waendelee kuwaombea yeye pamoja na Rais Magufuli na Makamu wake, Samia Suluhu Hassan ili waweze kutimiza malengo waliyoahidi kwa Watanzania wakati wa kampeni.