Waziri Mkuu Majaliwa Akuta ‘Madudu’ Hospitali ya Mawenzi Moshi

Hospitali ya Rufaa Mawenzi mjini Moshi, Kilimanjaro.

Hospitali ya Rufaa Mawenzi mjini Moshi, Kilimanjaro.

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amewasili mkoani Kilimanjaro na kufanya ziara kushtukiza kwenye hospitali ya rufaa ya Mawenzi ambayo ni hospitali ya mkoa huo. Waziri Mkuu Majaliwa ambaye mara baada ya kuwasili Ikulu ndogo ya Moshi mjini Januari 30, 2016 alipangiwa kupokea taarifa ya mkoa huo, alimweleza Mkuu wa mkoa huo kwamba anataka kufanya ziara katika hospitali hiyo na kuwaomba radhi watendaji waliokuwa wanasubiri taarifa ya mkoa iwasilishwe.

“Mheshimiwa Waziri Mkuu ameamua kufanya ziara katika hospitali ya rufaa ya Mawenzi ambayo ni hospitali yetu ya mkoa na atakuja kupokea taarifa ya mkoa wetu tukishatoka huko,” alisema Mkuu wa mkoa huo, Bw. Amos Makalla.

Mara baada ya kuwasili hospitalini, Waziri Mkuu alielekeza apelekwe kwenye chumba cha upasuaji (theatre) huku akimuuliza maswali kadhaa Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo, Dk. Bingileki Lwezaula. Katika chumba cha upasuaji ilibainika kuwa kuna vyumba vitatu vya kufanyia upasuaji lakini kinachotumika ni kimoja tu kwa sababu vingine havina dawa za kulaza wagonjwa wanaofanyiwa upasuaji (anesthesia) licha ya kuwa jengo la upasuaji lina mwaka sasa tangu lilipozinduliwa Februari, 2015 na Rais Mstaafu Jakaya Kikwete.

Akiwa katika wodi ya utabibu ya wanawake, Waziri Mkuu alipokea malalamiko kutoka kwa wagonjwa juu ya kukosekana kwa dawa hospitalini hapo. Afisa Muuguzi wa wodi hiyo, Bi. Anjela Mwakalile alisema wametuma maombi ya kupatiwa dawa kutoka MSD lakini bado hazijafika.

Hali hiyo ilijitokeza pia kwenye wodi ya watoto. Akizungumza na wazazi wa watoto aliowakuta wamelazwa, mama mmoja alimweleza Waziri Mkuu kwamba sera ya Taifa inasema watoto wachanga hadi walio na miaka mitano wanapaswa kupata matibabu bure, lakini wao hapo hospitalini wanalazimika kununua dawa. Waziri Mkuu alimtaka Mganga Mkuu wa Mkoa huo, Dk. Mtumwa Mwako kubadili haraka mfumo wa uagizaji wa dawa baada ya kupokea maelezo ya Dk. Lwezaula kwamba wametuma maombi MSD tangu miezi miwili iliyopita lakini hadi sasa hawajaletewa dawa walizoomba.

“RMO ni kwa nini hamuwezi kuagiza dawa nyingi (bulk) kwa magonjwa ambayo mnajua yanajirudia mara kwa mara ili wagonjwa weu wasipate usumbufu? Hii ni hospitali ya mkoa na mgao wa dawa unaopaswa kuja hapa ni wa level ya mkoa? Haiwezekani mnafanya hivyo ili wagonjwa wajinunulie dawa kutoka kwenye maduka yenu?,” alihoji Waziri Mkuu.

“Hii hospitali ni kubwa kuliko idadi ya wagonjwa wanaofika kutibiwa hapa na hii ni kwa sababu wengi wao wanaishia kwenye hospitali za wilaya. Kwa hiyo mlipaswa kuwa na dawa za kutosha. Wodini nimekuta wagonjwa wachache katika wodi nilizopita, ina maana mna ahueni hapa… mnao madaktari wa kutosha, wataalamu 12, lakini ni kwa nini hakuna dawa za kutosha?” alihoji.

Wakati akitoka wodi ya watoto, kijana mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Bakari Hussein ambaye anauguza mgonjwa wake hospitalini hapo alimweleza Waziri Mkuu kwamba dawa pekee wanayopatiwa kwenye hospitali hiyo ni paracetamol tu.

“Hapa dawa ya bure pekee unayopata ni paracetamol tu. Dawa nyingine zote unaandikiwa ukanunue maduka ya nje. Na ukizipata ni kati ya sh. 60,000/- hadi 70,000/- kwa mkupuo.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amemuagiza Katibu Tawala wa Mkoa wa Kilimanjaro, Bw. Severine Kahitwa apeleke maombi ya kupatiwa mafundi wa mashine za xray haraka iwezekanavyo kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.
Waziri Mkuu amefikia uamuzi huo baada ya kukuta mashine kubwa kwenye chumba cha mionzi cha hospitali haifanyi kazi na inayofanya kazi ni ndogo haiwezi kufanya baadhi ya vipimo.

Akitoa maelezo mbele ya Waziri Mkuu, Mkuu wa kitengo cha Radiolojia, Dk. Ephraim Minja alisema: “Tuliambiwa spare parts zimekwama bandarini, na vifaa hivyo vikipatikana vitaweza kutatua tatizo lililopo.”

Alipoulizwa na Waziri Mkuu kabla ya mashine ya kuharibika alikuwa akihudumia wagonjwa wangapi, Dk. Minja alisema kwa wastani alikuwa akihudumia wagonjwa 60 hadi 70. “RAS fuatilia mafundi kwa Katibu Wizara ya Afya. Hii ni hospitali kubwa tena ya Serikali kwa hiyo haiwezekani wagonjwa waje hapa na kuambiwa waende kupata vipimo mtaani,” alisema.