Waziri Mkuu Azindua Mradi wa Maji wa Bilioni 2.27

Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akizungumza.

Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akizungumza.


 
Na Mwandishi Wetu

WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda ameagiza wananchi wa mji wa Kibaigwa kutunza vyanzo vya maji vinavyopatikana katika Wilaya ya Kongwa ili kuendelea kupata huduma ya maji safi na salama ambayo ni huduma muhimu kwa mahitaji ya wananchi wa Wilaya hiyo.
 
Alisema hayo Machi 17, 2014 wakati akizindua rasmi Mradi wa Maji uliojengwa na Kampuni ya China Hunan uliochimba Visima viwili vya maji Safi na Salama vyenye urefu wa mita 101 katika Mji Mdogo wa Kibaigwa ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya wiki ya Maji ambayo hufanyika kila mwaka, na mwaka huu maadhimisho hayo kitaifa yanafanyika mkoani Dodoma. 
 
Akizungumza na wananchi waliohudhuria uzinduzi huo, Waziri Mkuu aliwaeleza kuwa  chanzo hicho cha maji ni muhimu na ni utajiri wa mji wa Kibaigwa ambao wananchi wa mji huo wameombwa kutunza vyema chanzo hicho kwa ajili ya matumizi yao ya kila siku.
 
“Ni meelezwa kuwa visima hivi vinauwezo wa kutoa maji lita 62 kwa saa“, Ni lazima mtafute njia ya kuwaeleimisha wananchi ili muweza kuhifadhi upatikanaji wa maji safi na salama katika mji wa Kibaigwa kwa kuangalia namna ya kujenga mazingira bora ya kutunza chanzo kile, alisema Waziri Mkuu. 
 
“Mradi huu ulianza kujengwa mwezi Machi 2011 na umekamilika mwezi Septemba, 2013 kabla ya mradi kuanza Mji mdogo wa Kibaigwa ulikuwa na wakazi wapatao 18,550 kati ya hao Wakazi 8,904 tu, sawa na asilimia 48 ndio walipata huduma ya maji, kwa mradi huu wa sasa asilimia 90 ya wananchi wa Kibaigwa wanauhakika wa kupata maji safi na salama na zaidi ya wananchi elfu 13,000 wanauwezo wa kupata huduma ya maji hayo,” alisema Waziri Mkuu.
 
“Hali ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama katika Wilaya ya Kongwa ni asilimia 68 ukiondoa mji mdogo wa Kibaigwa na sasa kuna miradi kumi katika vijiji kumi ambavyo ni Mkoka, Chigwengweli, Songambele, Malanje, Igangwa, Mseta, Mlali Iyengu, Mlali Bondeni, Ngumbi na Pembamoto, miradi hii ikikamilika itaongeza idadi ya watu wanaopata huduma ya maji Safi na Salama na kufikia asilimia 75 katika Wilaya ya Kongwa,” alisisitiza Waziri Mkuu.
 
Waziri Mkuu alisema, Miradi hii ni kiashiria kuwa Serikali kupitia Ilani yake ya Chama Cha Mapinduzi inatambua umuhimu wa sekta ya Maji kwa maendeleo ya Kiuchumi, Kijamii na hifadhi za mazingira, hivyo Serikali itahakikisha upatikanaji wa maji safi na salama kufikia asilimia 75 Vijijini na asilimia 95 Mijini ifikapo 2015.
 
Waziri Mkuu alisema; “nimesikia kuwa ndoo ya lita 20 ni sh 20, ndoo ya lita 10 ni sh 10 na pipa ni sh 250.” Kwa utaratibu huo ni vema uongozi wa Mji wa Kibaigwa kuangalia utaratibu wa kutunza fedha hizo kwani kutakuwa na matengezo na marekebisho ya mashine pale zitakapo haribika, pia aliwaomba kuanzisha utaratibu wa kutoa taarifa walau kila baada ya miezi mitatu ili wananchi kupafamau mapato na matumizi ya huduma ya maji inayotolewa.
 
Vilevile, Waziri Mkuu alisema Sera ya Maji ya mwaka 2002 inalenga katika kuhakikisha kuwa Wananchi Vijijini wanapata huduma ya maji safi na salama kwa umbali usiozidi Mita 400 kutoka kwenye makazi yao. Ii kufikia lengo hilo, Serikali kwa kushirikiana na Washirika wa Maendeleo, Serikali za Mitaa, Wananchi na wadau wengine itaendelea kuboresha huduma za maji vijijini kwa kujenga miradi mipya, kupanua na kukarabati miundombinu ya maji. 
 
Maadhimisho ya Wiki ya Maji yalianza mwaka 1992 ambapo iliamuliwa kuwe na kauli moja kuanzisha Wiki ya Maji Duniani. Mwaka huu Kimataifa yanafanyika Tokyo, Nchini Japan.