Waziri Mkuu Australia Ampongeza Rais Kikwete Kuachia Madaraka Kikatiba

Rais Jakaya Mrisho Kikwete akilakiwa na Waziri Mkuu wa Australia Mhe. Tonny Abbot alipowasili asubuhi ya tarehe  28 Julai 2015  katika makao  Makuu ya kiongozi  huyo  jijini Sydney

Rais Jakaya Mrisho Kikwete akilakiwa na Waziri Mkuu wa Australia Mhe. Tonny Abbot alipowasili asubuhi ya tarehe 28 Julai 2015 katika makao Makuu ya kiongozi huyo jijini Sydney

Rais Jakaya Mrisho Kikwete na ujumbe wake wakiwa katika mazungumzo rasmi na Waziri Mkuu wa Australia Mhe. Tonny Abbot asubuhi ya tarehe 28 Julai 2015 katika makao Makuu ya kiongozi  huyo jijini Sydney

Rais Jakaya Mrisho Kikwete na ujumbe wake wakiwa katika mazungumzo rasmi na Waziri Mkuu wa Australia Mhe. Tonny Abbot asubuhi ya tarehe 28 Julai 2015 katika makao Makuu ya kiongozi huyo jijini Sydney

Rais Jakaya Mrisho Kikwete akiongea wakati wa chakula cha mchana kwenye jumba la serikali jijini Sydney tarehe 28 Julai 2015 baada ya kukutana na kufanya mazungumzo na Gavana Mkuu wa Australia Mheshimiwa Peter Cosgrove. PICHA NA IKULU

WAZIRI Mkuu wa Australia, Tony Abbot amempongeza Rais Jakaya Mrisho Kikwete kwa kuamua kukabidhi madaraka kwa kiongozi mwingine kwa mujibu wa Katiba nchini Tanzania.

“Nakupongeza sana kwa uamuzi wako wa kukabidhi madaraka kwa amani nchini kwako , ni jambo la nadra sana Barani Afrika, kuwa na utaratibu mzuri na wa Amani namna hii” Bw. Abbot amemuambia Rais Kikwete na kumueleza awe na uhakika kuwa ” Australia itaendelea kuisaidia Tanzania katika juhudi zake za kuleta maendeleo na kukuza uchumi” ameongeza.

Rais Kikwete na Waziri Mkuu Abbot pia wamezungumzia jinsi nchi zao zinaweza kuendelea kushirikiana katika kulinda usalama baharini, kukuza zaidi ushirikiano wa kidiplomasia, kiuchumi na kijamii.

Rais Kikwete yuko nchini Australia kwa mwaliko rasmi wa Kiserikali kutoka kwa Gavana Mkuu wa Australia Mheshimiwa Peter Cosgrove.

Rais Kikwete amepokelewa leo asubuhi tarehe 28 katika makao Makuu ya kiongozi wa Australia kwa heshima zote kwa kupigiwa mizinga 21 na kuandaliwa chakula rasmi cha mchana na baadae kupanda mti kuashiria kuimarisha mashirikiano baina ya nchi hizi mbili kwa kipindi kirefu kijacho.

Tanzania na Australia zimedumu katika ushirikiano baina ya nchi zao tangu miaka ya sitini na sasa nchi mbili hizi zimeazimia kuimarisha mahusiano haya zaidi katika sekta mbalimbali zikiwemo za uwekezaji na biashara kati yao.

Baadae leo jioni Rais Kikwete atakutana na wawekezaji wakubwa wa Australia ambao tayari wanawekeza nchini Tanzania kwa ajili ya mazungumzo ya namna ya kuendeleza sekta mpya ya gesi nchini na jinsi Tanzania inaweza kunufaika kutokana na kupata gesi.

Tayari Serikali ya Australia na makampuni binafsi ya gesi na mafuta, yanaisaidia Tanzania hasa katika vyuo vya ufundi stadi VETA na tafiti mbalimbali katika Kilimo.

Kesho tarehe 29 Julai, 2015 Rais Kikwete anatarajia kutunukiwa digrii ya udaktari wa heshima ya Sheria kutoka Chuo Kikuu cha Newcastle, kwa mchango wake mkubwa alioutoa katika uongozi kwa kipindi cha miaka 10 aliyokaa madarakani nchini Tanzania na Dunia kwa ujumla. Rais Kikwete anatarajia kuondoka Australia na kurejea Tanzania baada ya shughuli ya kupokea shahada yake na ratiba yake kwa ujumla.