WAZIRI MKUU Mizengo Pinda ameagiza iundwe tume ya kuchunguza tuhuma za ubadhirifu kwenye mradi wa maji wa Nyumbigwa wilayani Kasulu mkoani Kigoma na kutaka apewe taarifa yake katika muda wa wiki mbili.
Ametoa agizo hilo Oktoba 4, 2013 wakati akizungumza na mamia ya wakazi wa kijiji cha Nyumbigwa kwenye uwanja wa michezo mara baada ya kuweka jiwe la msingi kwenye mradi huo wa
maji.
Waziri Mkuu ambaye yuko katika siku ya nne ya ziara yake mkoani
Kigoma, alimtaka Waziri wa Nchi (OWM-TAMISEMI), Bibi Hawa Ghasia aunde timu maalumu itakayoshirikisha uongozi wa mkoa, wilaya ya Kasulu na kijiji cha Nyumbigwa na kufuatilia tuhuma hizo ambazo zimetolewa na Mbunge wa Kasulu Mjini (NCCR-Mageuzi), Moses Machali.
Alipopewa fursa ya kusalimia wananchi kabala Waziri Mkuu hajazungumza na wakazi hao, Bw. Machali alidai kuwa ana wasiwasi na uhalisia wa mradi pamoja thamani ya fedha zilizotumika katika mradi huo kwani alipoomba BOQ kutoka Halmashauri ya Wilaya ili acheki mabomba yaliyotumika alinyimwa.
“Nimeambiwa na wananchi ninaowawakilisha kwamba mabomba yaliyotumika yana madaraja tofauti na yana bei tofauti… yapo ya class B, C, D na E. Kijiji kiliomba kupewa BOQ pia kikanyimwa. Sitashangaa kuona mabomba yakipasuka mara tu baada ya mradi kuanza kazi,” alisema.
Ili kuondoa utata huo, Waziri Mkuu alimwita Mhandisi wa Maji wa Wilaya hiyo, Bw. Mbaraka Rajab Ally aeleze ni kwa nini amemdanganya kwenye taarifa aliyotoa wakati akizundua mradi huo.
Akitoa majibu, Bw. Ally alisema hajadanganya kuhusu taarifa
aliyompatia na ana uhakika na taarifa yake. Kuhusu mabomba
yaliyotumika, Bw. Ally alisema: “Maji ya mradi ule ni ya mtiririko kwa hiyo yanahitaji mabomba ya saizi tofauti. Na yalivyotumika, ndivyo yalivyoainishwa kwenye andiko la mradi.”
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Bibi Dorothy Rwiza
alipoitwa na Waziri Mkuu athibitishwe ukweli wa madai ya Mbunge wa Kasulu, alijibu: “Maneno ya mbunge yana uongo kwa asilimia kubwa sana. Waziri Mkuu teua tume ije iangalie ukweli wa jambo hili,” alisema.
Akizungumza na wananchi wa kijiji hicho, Waziri Mkuu aliwaonya
Mkurungenzi na Mhandisi akisema: “Ole wenu Mkurrugenzi na Mhandisi muwe mmemdanganya Waziri Mkuu. Nitafuatilia ripoti ya tume itakayoundwa na Mama Ghasia,” alisema.
Waziri Mkuu alisema amesikitishwa na tuhuma hizo na kwamba kuna dalili kuwa uongozi mzima wa wilaya una kasoro kwani haiwezekani kuwe na tatizo kama hilo viongozi washindwe kufuatilia hadi wamsubiri yeye afike ndipo waanze kushtakiana.
“Mmenisononesha sana. Sikutarajia mkutano huu uwe ni sehemu ya
kushtakiana kuhusu mradi ambao tangu awali mlikuwa na nafasi ya
kuhojiana na kuufuatilia kwenye vikao vyenu. Mlipaswa kuulizana katika vikao vyenu na siyo kusubiri wakati umebakiwa wiki mbili kuanza kazi,” alisema.
“Mbunge ni diwani, wewe ni sehemu ya maamuzi. Nashangaa mbunge,
madiwani na Halmashauri wameona kasoro ya mradi halafu wanashindwa kuusimamia na kuufuatilia hadi unafikia hatua hii,” alihoji.
Katika ziara hiyo ya siku sita mkoani Kigoma, Waziri Mkuu amefuatana na mkewe Mama Tunu Pinda, Waziri wa Nchi (OWM-TAMISEMI), Bibi Hawa Ghasia; Waziri wa Kilimo na Chakula, Eng. Christoher Chiza; Naibu Waziri wa Maji, Dk. Binilith Mahenge; Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Bw. Lazaro Nyalandu pamoja na Naibu Waziri Nishati na Madini,
Bw. George Simbachawene.