WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda amesema uwiano wa kibiashara baina ya Tanzania na China hauko sawa kwa sababu Tanzania inauza nchini China bidhaa ambazo hazijasindikwa lakini inanunua kutoka huko bidhaa ambazo zimekamilika (finished products).
Ametoa kauli hiyo Septemba 10, 2013 wakati akifungua maonyesho ya bidhaa zinazozalishwa na kampuni za Kichina kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee. Maonyesho hayo yanayotarajiwa kufungwa Ijumaa, Septemba 13, mwaka huu, yanahudhuriwa makampuni zaidi ya 200 kutoka majimbo 14 ya China.
“Mazingira haya ya kibiashara hayaleti usawa wala maendeleo kwa nchi zote mbili, ni vema wawekezaji wa China wakaangalia uwezekano wa kujenga viwanda vya kusindika bidhaa hapa nchni ili Tanzania nayo iweze kuuza bidhaa zilizotoka viwandani badala ya zile ambazo hazijazisindikwa,” alisema.
Alisema hatua hiyo itaiwezesha Tanzania kuuza bidhaa zilizokamilika siyo tu hapa nchini, bali kwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki, Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika na Ukanda Huru wa Kibiashara (Free Trade Area) ambazo kwa ujumla wake soko lake lina watu zaidi ya milioni 750.
Alisema kufanyika kwa maonyesho hayo hapa nchini kunasaidia kuonyesha mbinu mpya za kiteknolojia kwa wajasiriamali na wafanyabiashara wa Kitanzania. “Tunahitaji kupata teknolojia za kisasa kutoka kwenu ili tuboreshe bidhaa zinazozalishwa nchini na ziweze kuuzika China na kwenye masoko ya kimataifa,” aliongeza.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kukagua mabanda mbalimbali, Waziri Mkuu alisema kimsingi maonyesho hayo ni mazuri na yamelenga kufuta hisia zilizopo kwa watu wengi juu ya ubora hafifu wa bidhaa zinazozalishwa China.
Hata hivyo, alisema ameona vitenge vya wax vinavyozalishwa China na kuongeza kuwa haoni sababu ni kwa nini pamba inayozalishwa nchini isitumike kutengeneza vitenge kama hivyo endapo watajenga kiwanda chao hapa nchini.
Mapema, Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Abdallah Kigoda alisema maonyesho kama hayo yatasaidia kuongeza biashara siyo tu kati ya Tanzania na China bali miongoni mwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Wakati huohuo, Balozi wa China nchini Tanzania, Dk. Lu Youqing alisema China imekuwa mshirika mkuu wa kibiashara baina yake na nchi za Afrika kwa muda wa miaka minne mfululizo. Kuhusu uwekezaji hapa nchini, Dk. Lu alisema mwaka jana China iliwekeza miradi yenye thamani ya dola za marekani bilioni moja na kati ya Januari na Juni mwaka huu, uwekezaji umefikia dola za marekani bilioni 2.17.
Alitaja maeneo makuu ambayo makampuni ya Kichina yanawekeza kuwa ni kwenye ujenzi wa barabara, umeme, kilimo, viwanda na mawasiliano.
Naye, Naibu Mkurugenzi wa Biashara za Nje katika Wizara ya Biashara ya China, Bw. Zhang Xialing alisema Tanzania na China zimekuwa zikishirikiana kwa muda mrefu katika masuala ya biashara. Alisema kwa mwaka 2012, biashara baina ya nchi hizo mbili iliongezeka kwa asilimia 50.2 na katika kipindi cha Januari hadi Juni 2013, biashara imeongezeka kwa asilimia 54.
Alisema maonyesho hayo yamedhaminiwa Serikali za Majimbo ya Shanghai, Jiangsu, Zhejiang na Guangdong kwa kushirikiana na Chama cha Wafanyabiashara wa Tanzania (TCCIA) pamoja na Baraza la Biashara Africa baina ya Tanzania na China.