Waziri Mkuu Ataka Bonde la Mto Mara Litunzwe

WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda


 
WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda amesema idadi kubwa ya mifugo katika bonde la mto Mara ni mojawapo ya changamoto zinazokabili utunzaji endelevu wa bonde na amewataka viongozi wa mkoa watoe elimu ya kutosha kwa wananchi ili wafuge kisasa na kuepusha uharibifu wa mazingira.
 
Ametoa kauli hiyo Septemba 15, 2013 wakati akifunga maadhimisho ya Siku ya Mara (Mara Day Celebrations) yaliyofanyika kwenye uwanja wa Sokoine mjini Mugumu, wilayani Serengeti mkoani Mara. Maadhimisho hayo yalianza Septemba 12, mwaka huu.
 
“Changamoto iliyopo ni kuainisha, matumizi bora ya ardhi iliyopo kwa kuzingatia uwiano baina ya ardhi na mifugo iliyopo. Tunawajibika kupima ardhi yetu kuanzia ngazi ya vijiji ili kuepusha athari zinazotokana na kuzidisha mifugo katika maeneo tuliyonayo ikiwemo eneo la Mto Mara.
 
“Kupima ardhi kutasaidia kuepusha migogoro inayoweza kutokea baina ya wakulima na wafugaji. Tutaendelea na mikakati ya kutoa elimu ya kutosha kwa wananchi ili wafuge kisasa na kupunguza idadi ya mifugo ili kuepuka uharibifu wa mazingira,” alisema.
 
Alisema bonde la mto Mara ni rasilmali kwa wakazi wa Mara na kwamba kama bonde hilo likitumiwa vizuri lina fursa kubwa ya kiuchumi na hasa kwenye kilimo cha umwagiliaji maji.
 
Alisema wastani wa pato la mwananchi wa Mara liko chini ikilinganishwa na mikoa jirani ya Mwanza, Manyara na Shinyanga na kwamba kilimo cha umwagiliaji kwa mazao kama mpunga na mbogamboga kitasaidia kuinua pato la wananchi wa mkoa huo.
 
“Ili kulitunza bonde hili ni lazima tuache kazi za kilimo umbali wa mita 60 kutoka kingo za mto huu kwa mujibu wa sheria. Tuache kuchoma misitu, tuache kukata miti hovyo, na kama mnataka kufanikiwa, nawashauri mfuge nyuki. Mkiwa na mizinga yenu kwenye misitu hamtachoma moto, ni lazima mtajizuia kuchoma moto ili msiwadhuru nyuki wenu,” alisema.
 
Alisema bonde la mto Mara ni fursa ya kisiasa, kijamii na kiuchumi hivyo wakazi wa bonde hilo wa pande zote mbili hawana budi kulitunza kwa faida ya kizazi cha sasa na cha baadaye. Aliwaomba viongozi wa Tanzania na Kenya kushirikiana kulitunza bonde hilo na kuhakikisha kwamba Mto Mara unadumu.
 
“Mto Mara ni mto wenye historia, ni mto wa kumbukumbu, ni mto wa shughuli za kiuchumi na shughuli za maendeleo. Lakini zaidi ya yote, mto Mara unaunganisha jamii za pande zote mbili Kenya na Tanzania. Tutumie mto Mara kama alama (Symbol) ya chanzo cha umoja wetu, mshikamano, udugu na upendo kati ya wananchi wa Kenya na Tanzania na hata nchi zote za maziwa makubwa zinazotumia Ziwa Victoria,” alisema.
 
Maadhimisho hayo yalihudhuriwa na Naibu Mawaziri wa Maji, Maliasili na Utalii na TAMISEMI pamoja na viongozi kadhaa kutoka Serikali ya Kenya. Pia wakuu wa mikoa ya Arusha, na Manyara, na wakuu wa wilaya mbalimbali.