Na Mwandishi Wetu, Dodoma
WAZIRI wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Bernard Membe amesema kuwa Serikali imetekeleza kwa kiwango cha juu mchakato wa tathmini ya utawala bora nchini (APRM) na kulipongeza Baraza la usimamizi la Taifa la APRM.
Waziri Membe aliyasema hayo mjini hapa wakati wa kuwasilisha bajeti yake ambayo baadaye ilipishwa na Bunge kwa kauli moja. Waziri alikuwa akieleza utekelezaji wa majukumu yake na taasisi zilizo chini ya Wizara yake.
“Mchakato wa APRM umeendelea vyema ambapo mwaka huu Serikali ilipokea timu ya wataalamu kutoka makao makuu ya APRM kwa ajili ya kuihakiki ripoti yetu,” alisema.
Aliongeza kuwa kazi ya tathmini ya utawala bora nchini ilifanyika kwa uadilifu mkubwa na akatambua kazi iliyokuwa ikifanywa kwa weledi na bodi ya APRM. Bodi ya APRM kwa sasa inaongozwa na Prof. Hasa Mlawa.
Wananchi wa kada mbalimbali wakiwemo wabunge wamekuwa wakitoa maoni mbalimbali kuhusu APRM wakisema kuwa katika kuboresha na kuinua utawala bora nchini ni vyema Serikali ikafanyiakazi tafiti mbalimbali zinazofanywa na taasisi zake hasa tafiti za utawala bora zinazofanywa na APRM.
APRM ni Mpango wa Bara la Afrika Kujitathmini Kiutawala Bora na hapa nchini taasisi hiyo imepewa dhamana ya kukusanya maoni ya wananchi kuhusu hali ya utawala bora ili kuisaidia Serikali kufanyiakazi changamoto zinazojitokeza.
“Naipongeza APRM kwa kazi nzuri na taasisi hii ni vyema ikaendelezwa ili kuisaidia nchi yetu kung’amua masuala mbalimbali ya utawala bora,” alisema mbunge Beatrice Shellukindo alipokuwa akichangia hoja Bungeni.
mmoja wa wananchi waliohudhuria banda la APRM akijitambulisha kuwa ni mwanafunzi wa chuo cha Mipango huku akihoji kama ripoti za APRM na tafiti nyingine zinatekelezwa na Serikali.
Akizungumza kwa niaba ya kambi ya upinzani Bunge, mbunge wa Nyamagana, Ezekia Wenje alisema taasisi ya APRM ni muhimu kutokana na ripoti zake za utawala bora lakini akashauri kuwa ni vyema Serikali ikaipa fedha za kutosha taasisi hiyo kufanyakazi zake.