Waziri Membe Akanusha Kuhusika Tukio la Kumdhuru Mhariri Kibanda

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe

WAZIRI wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe amekanusha madai ya kuhusika na vitendo vya kikatili alivyofanyiwa Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri, Absalom Kibanda.

Juzi gazeti la Mtanzania linalochapishwa na Kampuni ya New Habari 2006 Ltd, lilitoa habari inayomtuhumu Waziri Membe kuhusika na uhalifu huo, huku ikinukuu kauli zake alizotoa katika kipindi cha televisheni moja Julai mwaka jana, aliposema ana maadui kumi na moja kati yao wamo waandishi wa habari wawili.

Usiku wa kuamkia Machi 6, mwaka huu, Kibanda akiwa anarejea nyumbani kutoka kazini alivamiwa na watu wasiojulikana na kushambuliwa kiasi cha kuharibiwa jicho, kukatwa kichwa, kung’olewa meno na ukucha.

Hata hivyo akizungumza kupitia taarifa yake kwa vyombo vya habari, Membe alisema ameshangazwa na taarifa hizo na kusisitiza kuwa hahusiki.

“Nimeshangazwa na kusikitishwa na habari hizo, napenda niwahakikishie Watanzania wenzangu kwamba sijahusika, sikuhusika na sina sababu ya kuhusika kwa nanma yoyote ile,” alisema Membe na kuongeza:

“Sina nia, genge wala fedha za kufanya shughuli kama hiyo. Katika maisha yangu yote, sijawahi kugombana naye (Kibanda) na hajawahi kunifanyia ubaya wowote. Kwa kifupi sina uhasama na Kibanda.”

Membe anayetajwa kuwa mmoja wa watakaowania urais mwaka 2015 kupitia CCM, alisema habari hiyo ina malengo ya kisiasa.

“Huu ni mwendelezo wa mkakati wa kisiasa wa kunichafua ambao umekuwa ukiendelezwa na wale wasionitakia mema,” alisema.
Hata hivyo, Waziri Membe ambaye hivi karibuni alisema hatagombea tena ubunge, aliwashukuru watu waliomtumia salamu za kumtia moyo huku akihoji ujasiri wa watu wengine kusema uongo hadharani.

“Jeuri na kiburi cha namna hii hakiwezi kutokana na sheria za nchi, haki ya kikatiba wala hofu ya Mwenyezi Mungu. Naomba Watanzania wenzangu mnisaidie kutegua kitendawili hiki,” alisema Waziri Membe na kuongeza:

“Naamini ukweli kuhusu suala hili utajulikana na yeyote mwenye ushahidi aonyeshe uzalendo wake kwa kutoa taarifa kwenye vyombo vya ulinzi na usalama.”
Naye Ofisa Mkuu Mtendaji wa New Habari, Hussein Bashe alisema wao wanachotaka ni Waziri Membe ahojiwe kutokana na matamshi yake.

Bashe alidai kuwa, Waziri Membe analalamikiwa kwa mazungumzo yake kwenye kipindi katika kituo cha televisheni moja kudai ana maadui kumi na moja.
“Huyu bwana alitangaza ana maadui kumi na moja na kati ya hao wawili ni waandishi wa habari,” alisema Bashe.

Bashe aliongeza kuwa Waziri Membe alikwenda mbali zaidi na kudai angewashughulikia maadui zake.
“Sasa tayari kuna mwandishi ameumia na yeye (Membe) ana maadui waandishi ndiyo maana tunataka ahojiwe,” alisema Bashe.
Pia, aliongeza kuwa suala hilo lilijadiliwa kwenye kikao cha Wadau wa Vyombo vya Habari hivi karibuni.
CHANZO:Mwananchi