Waziri Mbarawa Awataka TEMESA Kuongeza Ujuzi Utengenezaji wa Vivuko

Kamishna Mkuu wa TGGA Tanzania, Symphorosa Hangi (kulia) akiwasalimia wanafunzi ambao ni wanachama wa Chama Cha Girl Guides Tanzania toka Temeke (TGGA) katika matembezi ya Maadhimisho ya TGGA kumuenzi mwanzilishi wa chama hicho Duniami, Roden Barden Powell yaliyofanyika Manispaa ya Temeke Dar es Salaam.

Meneja Mradi wa Kampuni ya Songoro Marine Transport inayotengeneza Kivuko cha MV. Kazi, Bw. Major Songoro, akitoa ufafanuzi wa mashine kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa, alipokagua Kivuko hicho jijini Dar es Salaam.

WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa ameutaka uongozi wa Wakala wa Ufundi na Umeme nchini (TEMESA) kushiriki kikamilifu shughuli za matengenezo ya vivuko ili kupata ujuzi wa ufungaji wa mifumo kutoka Kampuni zinazotengeneza vivuko vya Serikali.

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa kivuvko kipya cha MV Kazi, Bandarini jijini Dar es Salaam, Waziri Prof. Mbarawa amesema kuwa kupitia mafunzo hayo Serikali itaweza kuokoa fedha nyingi ambazo kwa sasa inatumia kulipa kampuni binafsi zinazojenga na kukarabati vivuko.

“Hakikisheni mnapata ujuzi kama walionao hawa, hatutaki kutumia fedha za Serikali kwa ajili ya kukarabati au kutengeneza vivuko wakati nyinyi TEMESA mpo,” amesema Waziri Prof. Mbarawa
Pamoja na ujenzi wa kivuko hicho Waziri Mbarawa amewataka Temesa kuhakikisha wanasimamia na kukitunza kivuko hicho ili kiweze kudumu kwa muda mrefu.

Aidha, Profesa Mbarawa ameuagiza Wakala huo kuhakikisha wanakamilisha mifumo ya ukusanyaji mapato kwa njia ya kielektroniki ili ili kudhibiti mianya ya rushwa.

Kuhusu huduma za kivuko mkoani Lindi Serikali imesema itahakikisha inapelekea huduma haraka iwezekanavyo ili kurahisisha usafiri kwa wananchi wa mkoa huo. Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Wakala huo Dkt. Musa Mgwatu, amemtaka mkandarasi wa kampuni ya Songoro Marine Transport kuhakikisha anafanya kazi usiku na mchana ili kukamilisha kivuko hicho kwa muda uliopangwa.

Dkt. Mgwatu amefafanua kuwa kukamilika kwa kivuko hicho kutarahisisha usafiri kwa wakazi wa Kigamboni na maeneo mengine ya jiji la Dar es salaam ambao wamekuwa wakitumia huduma hiyo katka shughuli zao za kila siku.

Nae, Meneja Mradi wa Kampuni ya Songoro Marine Transport, Bw. Major Songoro amemhakikishia Waziri Mbarawa kumaliza kivuko hicho kwa wakati ambapo amesema ifikapo tarehe 15 mwezi huu kivuko hicho kitakabidhiwa kwa Serikali.

Bw. Songoro amefafanua kuwa kwa sasa mafundi wanamalizia kazi ndogo ndogo zilizobaki ikiwa ni pamoja na kumalizia ufungaji wa injini. Kivuko kipya cha MV Kazi kimegharimu kiasi cha shilingi bilioni Saba na kina uwezo wa kubeba abiria 800 na magari 22 kwa wakati mmoja.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.