WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa ametoa miezi miwili kwa mkandarasi wa kampuni ya M/s Jiangxi Geo-Engineering (Group) Corporation anayejenga sehemu ya barabara ya Mangaka-Nakapanya yenye urefu wa Km 70.5 kukamilisha ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami.
Alisema hayo wakati akikagua ujenzi wa barabara ya Tunduru-Mangaka-Mtambaswala inayojengwa kwa kiwango cha lami yenye urefu wa Km 202.5 ambayo kukamilika kwakwe kutafungua fursa za kiuchumi na kuunganisha mikoa ya Ruvuma, Mtwara na Lindi. Amebainisha kuwa Mpango wa Serikali ni kuwajengea watanzania miundombili bora itakayowafikisha katika uchumi wa kati ifikapo 2025 hivyo haitamvumilia Mkandarasi anayechelewesha kukamilisha ujenzi wa miradi mbalimbali inayotekelezwa hapa nchini.
“Natoa miezi miwili mkandarasi uwe umemaliza hii barabara, wananchi wa Mangaka na Tanzania kwa ujumla wanahitaji kuanza kuitumia kwa ajili ya kuinua uchumi wa Taifa”, amesema Waziri Prof. Mbarawa.
Waziri Mbarawa ameongeza kuwa Serikali itaendelea kutoa fedha kwa Makandarasi wanaotekeleza miradi mbalimbali nchini hivyo lazima wajipange kumaliza kazi kwa wakati na kuzingatia viwango vya ubora kulingana na makubaliano ya mkataba. Aidha amesisitiza kuwa Serikali haitaingia mkataba mwingine kwa mkandarasi yoyote ambaye hatakamilisha kazi kwa wakati kulingana na makubaliano. Kwa upande wake Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) mkoa wa Mtwara Eng. Dotto John amemhakikishia Waziri Mbarawa kusimamia mradi huo ili ukamilike kwa wakati na kuchochea maendeleleo ya Mikoa ya kusini.
“Wananchi wamengojea kwa muda mrefu kukamilika kwa mradi huu ili uwe kichocheo cha maendeleo hivyo ninakuhakikishia kuwa nitawasimamia kwa umakini makandarasi ili wazingatie vigezo tulivyokubaliana kwenye mkataba”, amesisitiza Eng. Dotto.
Waziri Prof. Mbarawa amekagua mradi wa ujenzi wa barabara ya Tunduru-Mangaka-Mtambaswala yenye urefu wa km 202.5 inayojengwa kwa kiwango cha lami ambapo kukamilika kwake kutafungua fursa za kiuchumi mikoa ya Kusini ikiwemo kuiunganisha Tanzania na Msumbiji kwa lami kupitia daraja la umoja lililoko Mtambaswala.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano