WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa ameitaka Menejimenti ya Mfuko wa Mawasiliano kwa wote (UCSAF), kuhakikisha vijiji vyote nchini ambavyo havijaunganishwa na huduma ya mawasiliano vinaunganishwa kabla ya mwisho wa mwaka huu.
Aidha, Profesa Mbarawa amesisitiza mfuko huo kutoa kipaumbele kwa vijiji vyote vilivyomo sehemu za mipakani ili kuimarisha ulinzi na uharaka wa mawasiliano katika maeneo hayo. Amewaagiza UCSAF kukutana na mitandao ya simu ili kukamilisha kazi kwa mujibu wa mkataba kwa kata 121 ambazo hazijapata huduma ya mawasiliano hapa nchini.
“Nia ya Serikali ni kuhakikisha vijiji vyote nchini vinapata huduma ya mawasiliano ifikapo mwishoni mwa mwezi Novemba ili kuwezesha mikakati mingine ya kuboresha Mifumo ya Tehama katika shule na Hospitali kuendelea na hivyo kuhuisha huduma za Tehama katika Sekta za afya na elimu”, amesema Profesa Mbarawa.
Profesa Mbarawa ameonya kampuni za simu zitakazoshindwa kupeleka mawasiliano katika maeneo waliyopangiwa kwa wakati zitapokonywa masafa katika maeneo husika ili kuzipa kampuni zilizo tayari.
Naye Mjumbe wa Bodi ya UCSAF Bw. Godfrey Simbeye, amemhakikishia Waziri Mbarawa kuwa Bodi yake imejipanga kuhakikisha inaratibu huduma zote za Tehama zinazotolewa na taasisi mbalimbali nchini ili kuweka uwiano wa huduma hizo nchini kote. Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa UCSAF Eng Peter Ulanga, amesema kuwa mfuko huo umejipanga kupeleka mawasiliano katika maeneo yasiyo na mvuto kibiashara ili kutoa haki kwa wakazi wa maeneo hayo kunufaika na fursa za mawasiliano na kuchochea maendeleo.
Takribani asilimia 94 ya Wakazi wa Tanzania wanapata huduma ya mawasiliano lengo likiwa ni kufikia asilimia 100 ifikapo mwishoni mwa mwaka huu.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.