Waziri matatani Arumeru

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Nape Nnauye (kushoto) akimnadi mgombea wa ubunge wa chama hicho katika kampeni za uchaguzi mdogo wa Jimbo la Arumeru Mashariki, Sioi Sumari (katikati) kwenye mkutano uliofanyika katika Kijiji cha Ambureni jana.

VIJANA WA CHADEMA WAMZINGIRA, AHOJIWA NA POLISI

Waandishi Wetu, Arumeru

NAIBU Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Goodlucky Ole Medeye juzi usiku aliingia matatani baada ya kutiwa msukosuko na vijana wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), wakimtuhumu kujihusisha na utoaji rushwa kwenye kampeni za uchaguzi mdogo wa ubunge zinazoendelea Jimbo la Arumeru Mashariki.

Tukio hilo, lilitokea kati ya saa 12:30 jioni na saa 1.20 usiku eneo la Kata ya Mbuguni wilayani Arumeru, pale Naibu Waziri huyo alipokurupushwa na vijana hao, kisha kukimbilia Shule ya Msingi Oldevesi, kabla ya kuokolewa na polisi.

Taarifa kwamba Medeye amekamatwa, zilisambaa kwa kasi hali iliyosababisha watu kadhaa kwenda Kituo cha Polisi Usa River kupata taarifa kamili za tukio hilo, lakini ilifahamika kuwa, Naibu waziri huyo hakufikishwa polisi baada ya kutolewa Mbuguni.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, Thobias Andengenye akizungumza na Mwananchi kwa simu jana, alisema walipata taarifa kutoka kwa vijana hao juzi kwamba Naibu Waziri huyo alikuwa anafanya kampeni eneo la Shambarai.

Gazeti hili lilipomtafuta Naibu waziri huyo kupata ukweli wa tukio hilo, alikiri kukumbwa na mkasa huo, lakini alikanusha madai kwamba alikuwa akigawa fedha kwa lengo la kukisaidia Chama Cha Mapinduzi(CCM).

Hata hivyo, habari kutoka Mbuguni zilizolifikia Mwananchi, zilidai kuwa Medeye ambaye pia ni Mbunge wa Arumeru Magharibi, alikutwa na mkasa huo alipokuwa kwenye mazungumzo na mmoja wa wamiliki wa mashamba makubwa katika eneo hilo, mwenye asili ya kiasia (jina tunalihifadhi), pamoja na wanawake kadhaa ambao ni wakazi wa kata hiyo.

Baadhi ya vijana wanaodaiwa kuwa wafuasi wa Chadema, walimzingira Medeye na kuanza kumhoji sababu za kuwepo eneo hilo na kugawa fedha kwa lengo la kukisaidia CCM huku akitumia gari la Serikali, hali iliyozua tafrani na kusababisha Naibu Waziri huyo kutimua mbio hadi Shule ya Msingi Oldeves.

Wakati wakiendelea kujibizana, mmoja wa vijana hao alimpiga picha Naibu Waziri huyo pamoja na gari hilo lililokuwa na bendera ya taifa, na kwamba kitendo hicho kilimkera kiongozi huyo kiasi cha kutaka kuvunja kamera, hatua iliyochangia kuongeza kwa tafrani hiyo.

“Baada ya hali ya hewa kuchafuka, baadhi ya wakereketwa wa CCM walipiga simu Kituo cha Polisi Mbuguni, askari wakafika mara moja na kuondoka na Medeye hadi Kituo cha Polisi Mbuguni,” alidai mmoja kati ya mashuhuda wa tukio hilo.

Ilikuwaje?

Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Zanzibar, Hamid Mussa Yusuph, ambaye alikuwa eneo la tukio, alisema wakiwa katika kazi ya kutangaza mikutano ya chama chao juzi, waliona gari la waziri huyo na walipolisogelea, walimkuta akiwa jirani huku akizungumza na mkulima huyo mwenye asili na kiasia na baadhi ya akina mama.

“Sisi tulimhoji anafanya nini jioni katika eneo hilo akiwa na gari la Serikali? Akatujibu ana shughuli zake, hapo yakatokea majibizano, ndipo alikimbia kwenda kujihifadhi Shule la Oldevesi,” alisema Yusuph.

Alisema kutokana na idadi ya watu kuendelea kuongezeka katika eneo hilo, yeye (Yusuph) aliamua kupiga simu polisi, kuwaarifu na kwamba baada ya muda mfupi, askari walifika na baada ya kumhoji sababu za yeye kuwepo hapo, waliondoka naye. Inaendelea….
CHANZO: Mwananchi, kusoma zaidi habari hii bofya http://www.mwananchi.co.tz